WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema vyombo vya ulinzi na usalama nchini vimeendelea kufanya kazi ya kudhibiti matukio mbalimbali ya vitendo vya kihalifu ukiwemo wizi wa mifugo.
Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Septemba 9, 2021) wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbulu Vijijini, Flatei Massay katika kipindi cha Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu Bungeni jijini Dodoma.
Mbunge huyo alitaka kujua Serikali imejipangaje katika kudhibiti na kukomesha matukio ya wizi wa mifugo yanayotokea katika maeneo mbalimbali nchini.
Waziri Mkuu amesema mbali na hatua zinazochukuliwa na vyombo vya ulinzi na usalama pia, Serikali inawashirikisha wananchi katika ulinzi shirikishi ili kudhibiti vitendo hivyo.
“Tumedhibiti sana usafirishaji holela wa mifugo ikiwemo ng’ombe kutoka eneo moja kwenda lingine. Ng’ombe sasa hawezi kusafirishwa kwenda lingine bila ya kuwa na kibali maalumu.”
Amesema Serikali imeendelea kuwaelimisha wafugaji kufuga kulingana na ukubwa wa maeneo yao pamoja na kujenga mabanda imara ya kufugia mifugo yao.
Pia, Waziri Mkuu amesema katika kukabiliana na wizi wa mifugo Serikali imeanzisha mfumo wa utambuzi wa ng’ombe kwa kutumia hereni za kielektroniki ambao unaonesha mliki wa mfugo na eneo, hivyo kurahisisha utambu