Mkurugenzi wa Uhamasishaji na
Uwezeshaji wa Uwekezaji wa EPZA akitoa mada iliyohusu fursa zinatolewa
na maeneo maalum ya uwekezaji na namna ambavyo Serikali za mitaa na
biashara ndogo na za kati zinavyoweza kunufaika.
Mmoja ya wadau akiwa makini kusoma kijarida cha EPZA wakati wa majadiliano hayo yakiendelea.
Wadau wa uwekezaji, wafanyakazi wa
Taasisi ya Uongozi pamoja na wafanyakazi wa EPZA wakifuatilia kwa
makini hotuba ya Waziri wa Viwanda na Biashara Profesa Kitila
Mkumbo(hayupo pichani.)
Waziri wa Viwanda na Biashara
Prof. Kitila Mkumbo akiwa katika picha ya pamoja na wadau mara baada ya
kufungua majadiliano yaliyohusu uhusiano baina ya maeneo maalum ya
uwekezaji na uchumi wa ndani ambapo wadau mbalimbali wanaojihusisha na
masuala ya uwekezaji wameshiriki
…………………………………………………………..
Waziri wa Viwanda
na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo (MB) amewataka wadau wote hususan
Taasisi za Serikali wanaohusika katika kuwezesha uwekezaji wa viwanda
katika maeneo maalumu ya uwekezaji, kuhakikisha uwekezaji katika maeneo
hayo unafanyika kwa ufanisi kama ilivyokusudiwa kwa mujibu wa sheria na
taratibu zilizowekwa bila kufanya taratibu hizo kuwa kikwazo katika
uwekezaji.
Prof. Kitila
Mkumbo aliyasema hayo wakati akifungua kongamano la mahusiano kati ya
maeneo maalumu ya uwekezaji na uchumi wa ndani lililoandaliwa na Taasisi
ya Uongozi Tanzania (Uongozi Institute,) pamoja na Mamlaka ya Maeneo
Maalumu ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) lililofanyika Juni 19,
2021 jijini Dar es salaam.
Akifungua
Kongamano hilo, Prof. Mkumbo alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeweka
kipaumbele katika uendelezaji wa Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (SEZ). Aidha
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26
unasisitiza ustawishaji wa viwanda kwa maendeleo ya kiuchumi na watu kwa
lengo la kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2025 (TDV 2025)
inayolenga kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi shindani na endelevu
ifikapo mwaka 2025.
Aidha, Prof.
Mkumbo alisema Wizara ya Viwanda na Biashara imejipanga kuendeleza
viwanda vya kimkakati vinavyounganisha sekta mbalimbali, kuvutia na
kuwezesha uanzishwaji na upanuzi wa viwanda vinavyotoa ajira kwa watu
wengi, vinavyotumia malighafi zinazozalishwa hapa nchini hususani
kuongeza thamani katika mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi, misitu, na
madini ili kuongeza ushiriki wa wananchi katika ujenzi wa uchumi wa
viwanda, kuongeza kipato, na kuleta uwiano mzuri wa kiuchumi na kijamii
mijini na vijijini.
Prof. Mkumbo pia
alianinisha baadhi ya masuala muhimu ambayo mwekezaji huyazingatia kabla
ya kuwekeza katika maeneo maalumu kuwa ni pamoja na Masoko ya uhakika
ndani ya Tanzania na nje ya Nchi, Upatikanaji wa ardhi nzuri isiyokuwa
na migogoro ya umiliki wala athari kwa mazingira, Uwepo wa miundombinu
ya ndani (on-site infrastructure) kama barabara, maji, umeme na
mawasiliano na uwepo wa nishati ya uhakika kwa maana ya umeme na gesi
inayopatikana kwa bei ushindani,
Masuala muhimu
mengine yaliyoainishwa ni pamoja na Upatikanaji wa rasilimali watu wenye
ujuzi na stadi zinazoendana na shughuli wanazofanya viwandani na kwa
gharama itakayoweza kuwapa ushindani,Miundombinu ya uchukuzi kuingiza
malighafi viwandani na kutoa bidhaa zinazozalishwa kuelekea katika
masoko mbalimbali na Vivutio vya uwekezaji vya kifedha (“fiscal
incentives”) na visivyo vya kifedha (“non-fiscal incentives”) sambamba
na utulivu wa nchi kisiasa na kiusalama.
Prof. Mkumbo
alisema, katika kuhakikisha uchumi wa nchi unashindana kimataifa
Serikali inaendelea kujiunga na jumuiya mbalimbali za kikanda na
kimataifa kama vile Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya
Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ili kushindana kimataifa ili
kuimarisha biashara ndani ya Afrika na nje ya mipaka kwa kuweka
mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kukuza
uchumi wa taifa.
”Serikali
imejipanga kisera na kisheria kutoa huduma muhimu katika maeneo ya
uwekezaji, ujuzi muhimu katika elimu ili kwenda na matakwa ya soko kwa
ujumla pamoja na sheria za kodi katika kuhakikisha uwepo wa uzalishaji
wenye tija katika maeneo ya uwekezaji wa viwanda.” Alisema.
Aidha, Waziri
aliiagiza EPZA kuongeza bidii ya kuelimisha umma kuhusu dhana ya Maeneo
Maalumu ya Uwekezaji na kutangaza fursa na manufaa yanayotokana na
uwekezaji huo pamoja na kujifunza kutokana na uzoefu wa nchi nyingine
zinazofanya mageuzi ya kiuchumi nchini mwao kwa kujenga uchumi wa
viwanda kupitia Maeneo Maalumu ya Uwekezaji, na kuleta uzoefu huo nchini
kwa kuzingatia mazingira ya nchi yetu.
Serikali
imejipanga katika ujenzi wa mitaa ya viwanda “Industrial parts” pamoja
na kutangaza fursa za uwekezaji katika maeneo ya uwekezaji ya Kurasini,
Bagamoyo na Benjamin Mkapa mkoani Dar es Salaam ili kuhakikisha SEZ
zilizopo zinatimiza malengo yaliyokusudiwa ya kukuza uchumi imara wa
viwanda na kuimarisha ustawi wa wananchi ifikapo mwaka 2025. Alisema
Prof. Mkumbo.
Kwa upande wake
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Uzalishaji kwa Mauzo
ya Nje (EPZA,), John Mnali alisema Mamlaka hiyo imekuwa ikitekeleza
majukumu katika maeneo ya uwekezaji kwa niaba ya Serikali kwa
kuhakikisha maeneo yote ya uwekezaji yanapata huduma muhimu
hasa miundombinu ya maji, umeme na barabara pamoja na kutoa leseni za
uwekezaji kwa wawekezaji hao.
Kongamano hilo
lilijumuisha wawakilishi wa Serikali za Mitaa, Viwanda vidogo na
Biashara ndogo na kati, Kampuni za uwekezaji, Taasisi za Fedha, Wizara
ya Fedha na Mipango pamoja na Wizara ya Viwanda na Biashara walio
kujadili fursa za uwekezaji wa viwanda kupitia Maeneo Maalumu ya
Kiuchumi (Special Economic Zones (SEZ)), kuainisha changamoto
zinazohusiana na uwekezaji katika maeneo hayo na kuzitafutia ufumbuzi.
Aidha, Washiriki
wa kongamano hilo walitembelea Benjamin William Mkapa Special Economic
Zone ambayo ni eneo maalumu na mahususi kwa viwanda vinavyozalisha
bidhaa kwa mauzo ya nje ya nchi iliyojengwa na Serikali ya Awamu ya Tatu
ili kuona mandhari yake, shughuli zinazofanyika na kujifunza kwa
vitendo namna uwekezaji katika eneo hilo unavyochangia katika ukuaji
uchumi wa ndani.