Waziri mkumbo afanya ziara kukagua maandalizi ya maonesho ya 45 ya ditf (sabasaba) jijini dar es salaam

 

 

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) Mhe. Balozi Mteule Edwin
Rutageruka akizungumza kumkaribisha Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.
Prof. Kitila Mkumbo alipotembelea taasisi iliyo chini ya wizara yake ya
(Tantrade).

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.
Prof. Kitila Mkumbo (Mb) akizungumza na Menejimenti na wafanyakazi wa
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) alipotembelea
taasisi hiyo.

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.
Prof. Kitila Mkumbo (Mb) akizunguka katika mabanda mbalimbali kukagua
matayarisho ya Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam
yanayotarajia kuanza tarehe 28 Juni, hadi 13 Julai, 2021 katika Uwanja
wa Maonesho wa Mwl. J.K. Nyerere, Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam.

…………………………………………………………………………

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.
Prof. Kitila Mkumbo (Mb) amefanya ziara ya kutembelea taasisi ya Mamlaka
ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) ambapo amekutana na
kuzungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara
Tanzania (TanTrade) Mhe. Balozi Mteule Edwin Rutageruka na kujadiliana
namna ya kuboresha Maonesho ya mwaka huu na miaka ijayo kuwa mazuri na
yakuvutia hasa katika kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa
bidhaa za Tanzania.

Mhe. Prof. Mkumbo ameyazungumza hayo
leo tarehe 14 Juni, 2021 alipotembelea TanTrade na kukagua matayarisho
ya Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam
yanayotarajia kuanza tarehe 28 Juni, 2021 hadi 13 Julai, 2021 katika
Uwanja wa Maonesho wa Mwl. J.K. Nyerere, Barabara ya Kilwa, Dar es
Salaam.

Mhe. Prof. Mkumbo amesema kuwa Lengo
la Maonesho ya mwaka huu ni kutoa fursa kwa wafanyabiashara wa ndani na
nje ya nchi pamoja na taasisi mbalimbali kutangaza biashara, bidhaa na
huduma, kujifunza masuala ya biashara na teknolojia bora za uzalishaji
wa bidhaa kulingana na soko la kimataifa, kutengeneza mitandao ya
mawasiliano itayowasaidia kukuza biashara na kupata wabia wa biashara
ili kufikia malengo waliyojiwekea.

Aidha Mhe. Prof. Mkumbo amekagua
maeneo mbalimbali na kuridhishwa na kasi ya maandalizi ya Maonesho ya
mwaka huu na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kutembelea maonesho
ya mwaka huu yenye kauli mbiu isemayo “Uchumi wa Viwanda kwa Ajira na
Biashara Endelevu” ikilenga kutambua mchango wa Sekta ya Viwanda katika
kuchochea uzalishaji kwenye sekta mbalimbali za kiuchumi ikiwemo sekta
ya kilimo katika kukuza biashara ya ndani na nje, kuongeza ajira na
hivyo kuchangia kukua kwa uchumi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) Mhe. Balozi Mteule
Edwin Rutageruka amezikaribisha taasisi mbalimbali za ndani na nje ya
nchi kujiandaa kushiriki maonesho ya mwaka huu kwani kutakuwa na
Mikutano ya Kibiashara (B2B) ambayo itafanyika kwa njia za kidigitali
(Zoom Meetings) ili kuwakutanisha wadau wa ndani na nje ya nchi kwa
lengo la kuwatafutia masoko ya bidhaa na huduma mbalimbali.

Mhe. Balozi Mteule Edwin Rutageruka
amesema kuwa kutakuwa na huduma ya Kliniki ya Biashara, ambayo itatolewa
kwa wafanyabiashara ili kuboresha na kuimarisha mazingira wezeshi ya
ukuaji endelevu wa biashara ambayo itatolewa kwa kushirikiana na Taasisi
za Umma na Binafsi zenye Mamlaka za Uthibiti na Uwezeshaji wa Biashara.

Pia TanTrade imetenga eneo maalum
litakaloitwa ”Mtaa wa Kilimo” kwa lengo la kuwashirikisha wadau wa sekta
ya kilimo zikiwemo Bodi za Mazao, wazalishaji wa pembejeo na teknolojia
za kilimo pamoja na wadau wengine wa ndani na nje ya nchi ili
kurahisisha upatikanaji wao katika eneo moja na kuwaunganisha na masoko
endelevu.

Aidha, Mhe. Rutageruka amesema kuwa
kutakuwepo na “Mtaa wa Madini” utakaowashirikisha wadau wote wa sekta ya
madini kuanzia wachimbaji wadogo na wakubwa, watafiti na masonara kwa
lengo la kupanua fursa za masoko kwa sekta hii muhimu kiuchumi.

Mhe. Balozi Rutageruka amesema kuwa
usajili wa ushiriki wa maonesho ya mwaka huu unafanyika kupitia tovuti
ya TanTrade ambayo ni www.tantrade.go.tz au kutembelea Ofisi za TanTrade zilizopo katika Uwanja wa Maonesho wa Mwl J.K. Nyerere Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam.

MWISHO.