Nic yatoa msaada wa futari kwa watoto yatima na wajane jijini mwanza

 

NA MWANDISHI WETU


Shirika
la Bima la Taifa (NIC) limetoa msaada wa vitu mbalimbali kwa watu wenye
mahitaji maalumu hasa watoto yatima na wajane jijini Mwanza.


Akizungumza
wakati wa futari, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Dkt. Elirehema
Doriye amesema zoezi la kushiriki futari na kutoa zawadi kwa wahitaji
katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhan litafanyika katika mikoa minne
ambapo mpaka sasa wameshakwenda katika mikoa ya Tanga, Tabora, Mwanza na
watamalizia katika Mkoa wa Dar es Salaam.


“Kwa
mwaka huu tutafanya kwenye mikoa minne lakini mwakani tutaongeza zaidi
ili kuwafikia waislamu wengi zaidi na kushiriki katika ibada”. Amesema
Dkt.Doriye.


Aidha,
Dkt.Doriye amesema wameamua kufanya hivyo kwasababu ni muhimu kwao
kurudisha katika jamii kwani wanachokipata kinatoka katika jamii ambayo
wanaifanyia huduma hiyo na imewawezesha kufikia mafanikio hayo.


Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.John Mongella alilipongeza
Shirika la Bima la Taifa NIC kwa kutoa msaada kwa wahitaji pamoja na
kushiriki Futari katika mwezi huu wa ibada kwa waislam kote Duniani.


“Shirika
la Bima lilipotea katika ramani sasa naliona linafufuka linakuja tena
kwenye soko la bima na wote tuliopo hapa ndio washirika kwahiyo hii sio
hasara ni uwekezaji na ninaamini italipa tu kwa maana imefanyika katika
mazingira yenye baraka”. Amesema RC Mongella.


Pamoja
na hayo RC Mongella amezitaka taasisi zingine pamoja na watu binafsi
kuiga mfano uliofanywa na Shirika la Bima la Taifa NIC kwa kuwa mstari
wa mbele kutoa msaada kwa watu wenye mahitaji ili kwa pamoja tuweze
kuinyanyua jamii yetu.