Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud, amewasili kisiwani Pemba kwa ziara rasmi ya kikazi leo Aprili 29, ambapo amewasihi watendaji wote walio chini ya Ofisi yake kisiwani humo kufanya kazi kwa uadilifu na ufanisi wa hali ya juu.
Mapema leo amepokelewa katika Uwanja wa Ndege wa Pemba na viongozi wa kiserikali wakiongozwa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba na ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Micheweni, Mohammed Seif, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na viongozi na wanachama wa chama cha ACT Wazalendo.
Mara baada ya kuwasili, Makamu huyo wa Kwanza alikutana na baadhi ya watendaji wa Idara zilizo chini ya Ofisi yake, ambazo ni Mazingira, Watu Wenye Ulemavu, Tume ya Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya na Tume ya Ukimwi, kwa lengo la kutambuana na kubadilishana mawazo. Kikao hicho kilifanyika katika Ukumbi wa Wizara ya Fedha uliopo Gombani, kando kidogo ya Mji wa Chake Chake.
Katika kikao hicho, Mheshimiwa Othman amesisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii pasi na kuangalia wadhifa wake au anafahamiana na kiongozi gani.
“Hizi ni taasisi za serikali. Wananchi wanataka huduma na sisi ndio tunapaswa kuwahudumia. Tufanyeni majukumu yetu kwa nia moja ya kuisaidia serikali na wananchi wake. Mambo mengine ya itikadi tuyaache kando”, alieleza Makamu wa Rais Othman.
Aidha, amewataka viongozi wa idara hizo kuishi vyema na watendaji wao katika idara na wasijifakharishe na kuwadharau wengine, kwani yeyote anaweza kuteuliwa ama kuondolewa katika nyadhifa muda wowote.
“Tunatakiwa kuishi na watendaji wenzetu vyema ili kuongeza ufanisi wao. Tuwakosoe kwa busara wanapokosea na tuwapongeze wanapofanya vyema ili kuzisaidia taasisi na serikali”, alisema huku akisisitiza haja ya kila mmoja kutekeleza majukumu yake bila kushinikizwa.
Akiwa kisiwani Pemba, Mheshimiwa Othman atapata pia fursa ya kuwatembelea na kuwajulia hali wananchi wanaokabiliwa na mitihani mbalimbali, wakiwemo wagonjwa, wazee na watu wasiojiweza, ikiwa ni muendelezo wa ziara yake kama hiyo aliyoianza kisiwani Unguja.