Waziri ndaki awataka wafugaji kusimamia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya malisho

 

Waziri
wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akisaini kitabu cha wageni
ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro wakati alipofika mkoani hapo kwa
ajili ya kufungua mkutano wa kumi na moja (11) wa siku ya Nyanda za
Malisho Tanzania utakaofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Edema. Kulia
ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Loata Ole Sanare. (21.04.2020)



Mkurugenzi
wa Idara ya Uendelezaji Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya
Mifugo (WMUV), Dkt. Asimwe Rwiguza akisoma taarifa kwa niaba ya Katibu
Mkuu Mifugo kwenye mkutano wa kumi na moja (11) wa siku ya Nyanda za
Malisho Tanzania uliofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Edema mkoani
Morogoro.



Waziri
wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akifungua mkutano wa kumi na
moja (11) wa siku ya Nyanda za Malisho Tanzania ambapo wamewataka
wafugaji kuhakikisha wanasimamia na kuyatunza maeneo yaliyotengwa kwa
ajili ya shughuli za ufugaji. Mkutano huo umefanyika kwenye ukumbi wa
Hoteli ya Edema mkoani Morogoro.



Baadhi
ya Viongozi na wajumbe wa mkutano wa kumi na moja (11) wa siku ya
Nyanda za Malisho Tanzania wakisikiliza Hotuba ya ufunguzi ya mgeni
rasmi ambaye ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki. Mkutano
huo umefanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Edema mkoani Morogoro.



Waziri
wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akimkabidhi Mkurugenzi Msaidizi
Idara ya Uendelezaji Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya
Mifugo (WMUV), Rogers Shengoto (kulia) Kitabu cha Mpango Mkakati wa
Kwanza wa Utekelezaji wa Malengo ya Chama cha Malisho Tanzania wa Miaka
Mitano 2021-2025 kwenye mkutano wa kumi na moja (11) wa siku ya Nyanda
za Malisho Tanzania uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Edema mkoani
Morogoro.



 Waziri
wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amewataka wafugaji kusimamia maeneo
yaliyotengwa kwa ajili ya wafugaji na kuhakikisha wanayatunza.


Ndaki
ameyasema hayo jana (21.04.2021) wakati akifungua mkutano wa kumi na
moja (11) wa siku ya Nyanda za Malisho Tanzania uliofanyika katika
ukumbi wa Hoteli ya Edema katika mkoani Morogoro.


Wafugaji
wametakiwa kuhakikisha wanayasimamia na wanayatunza maeneo yote
yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za ufugaji na kuyaendeleza kwa
kupanda malisho na kuweka miundombinu ya maji kwa ajili ya kunyweshea
mifugo yao.


“Ni
lazima maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za ufugaji tunayalinda
na kuyaendeleza kwa kupanda malisho na kuweka miundombinu ya maji na
siyo kuyaacha yabaki kama mapori kwani watumiaji wengine wa ardhi
wanaweza kuanza kuyatumia na baadae migogoro inaanza,” alisema Ndaki.


Ndaki
pia amewataka wafugaji kuhakikisha wanaendelea kuomba ardhi kwa ajili
ya shughuli za ufugaji katika vijiji na kumilikishwa kwa kupata hati za
kimila ili waweze kuwa na maeneo kwa ajili ya mifugo yao lakini pia
waweze kupanda malisho.


Akizungumza
katika mkutano huo Waziri Ndaki amesema viongozi ni lazima wabadili
fikra pale wanapoona mifugo imeingia katika maeneo yao, badala ya
kulalamika inatakiwa watafute suluhisho kwani uwepo wa mifugo ni fursa
kiuchumi katika maeneo yao.


Vilevile
amewataka wataalam kuendelea kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu umuhimu wa
kumiliki ardhi na upandaji wa malisho kwa ajili ya mifugo yao.


Ndaki
amekishukuru Chama cha Nyanda za Malisho Tanzania kwa kazi nzuri
wanayoifanyana na amewahakikishia kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi
itaendelea kuwapa ushirikiano kwani malisho kwa mifugo ni jambo la
muhimu.


Naye
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Sanare amesema kuwa mkoa wake kwa
asilimia kubwa una wafugaji na wakulima lakini tatizo kubwa lililopo ni
watu kupata ardhi bila kufuata utaratibu, hata kwenye maeneo ambayo
tayari yalishapimwa na kutengwa kwa ajili ya shughuli za kilimo, mifugo
na watumiaji wengine wa ardhi.


Sanare
amesema kwa sasa wanaendelea kuwadhibiti watu ambao wanavamia ardhi
bila kufuata utaratibu ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua viongozi
kwenye vijiji na wataalam ambao wametoa hati za kimila bila kufuata
utaratibu au kwa kutojiridhisha.


Akisoma
taarifa kwa niaba ya Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Mifugo,
Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Maeneo ya Malisho na Rasilimali za
Vyakula vya Mifugo, Dkt. Asimwe Rwiguza amesema wizara imekuwa
ikishirikiana na Chama cha Nyanda za Malisho na wataalam katika
utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya uendelezaji nyanda za malisho hapa
nchini.


Dkt.
Rwiguza amesema wameshirikiana na chama hicho katika maandalizi ya
Mwongozo wa Upatikanaji, Usimamizi na Uendelezaji wa Maeneo ya Malisho
ambapo mwongozo huo upo katika hatua za mwisho ili uweze kuwasilishwa
kwa wadau kwa ajili ya kupata maoni yao.


Wizara
kwa kushirikiana na wadau ikiwemo Chama cha Nyanda za Malisho
imeendelea kutatua migogoro mbalimbali ya ardhi inayowahusu wafugaji na
watumiaji wengine wa ardhi. Vilevile Dkt. Rwiguza amewasihi wafugaji
kuhakikisha wanayatumia Mabaraza ya Ardhi ya Kata pale wanapokuwa na
migogoro ya ardhi.


Mwenyekiti
wa Chama cha Nyanda za Malisho Tanzania, Dkt. Ismail Selemani
amemshukuru Waziri kwa kukubali mwaliko wao na kushiriki katika kikao
hicho. Lakini pia amesema kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kila mwaka
imekuwa ikiendele kutatua changamoto mbalimbali zinazohusiana na Nyanda
za Malisho.


Dkt.
Selemani amesema kupitia wizara wanashuhudia kasi ya uanzishwaji wa
viwanda vya kuchakata mifugo na mazao yake hali ambayo itasaidia kukuza
uchumi wa wafugaji na kuongeza mchango wa mifugo katika pato la taifa.