Na Claud Gwandu,Arusha
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la International Evangelism lililopo Sakila wilayani Arumeru, Eliud Issangya amemtaka Rais Samia Suluhu Hassan kufuata nyayo za mtangulizi wake Hayati Dk John Pombe Joseph Magufuli
Rais Samia ameapishwa leo asubuhi ikulu jijini Dar es Salaam kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuchukua nafasi ya Hayati Dk John Pombe Joseph Magufuli ambaye alifariki Machi 17, mwaka huu kutokana na ugonjwa wa moyo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini hapa leo,Askofu Mkuu Issangya amesema kuwa ni vema Rais Samia akafuata nyayo za Dk Magufuli ili kuendeleza miradi mbalimbali ya kijamii iliyoanzishwa na mtangulizi wake huyo.
“Amefanya kazi na Dk Magufuli kwa miaka sita.Ana maono ya Dk Magufuli na lazima afuate nyayo zake kwa kuendeleza kwa nguvu na kasi ile ile miradi yote inayoendelea hivi sasa nchini kote.
‘’Iwe katika elimu aendelee na sera ya kutoa elimu bure kwa watoto maskini wa Tanzania au katika afya, ahakikishe hospitali,vituo vya afya na zahanati nyingi zinazojengwa nchini kote,zinakamilishwa na nyingine zinajengwa hiyo itakuwa heshima na urithi wa kudumu kwa Dk Magufuli,”anasisitiza Asofu Mkuu Issangya.
Anaongeza kuwa lazima Rais Samia ahakikishe miradi mikubwa ya kimkakati kama ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR, Bwawa la kuzalisha Umeme la Rufiji,usambazaji wa umeme vijijini ambayo ilikuwa sehemu ya maono aliyoishi nayo, inaendelezwa kwa kasi ile ile kwa manufaa mapana ya taifa.
Askofu Mkuu huyo pia alimtaka Rais Samia kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa,kutowavumilia watendaji wabovu serikali, kuwatetea wanyonge ili kumuenzi Hayati Dk Magufuli ambaye anatarajiwa kuzikwa nyumbani kwake Chato mkoa wa Geita wiki ijayo
“Tulipokea tangazo kwa kifo cha Rais wetu shupavu kwa mshtuko mkubwa na masikitiko mengi, kwa sababu ni tukio kubwa na halijawahi kutoke katika historia ya nchi yetu.Sawa,limetokea na hatuna la kufanya lakini daima tutamkumbuka Dk Magufuli kwa mambo mengi aliyotufanyika, kama taifa katika muda mfupi wa uongozi wake.
“Kwa niaba ya waumini wa kanisa la International Evangelism,tunatoa salamu za pole kwa watanzania wote,na kwa kuwa Dk Magufuli alikuwa mtu wa Imani,tuna hakika Mwenyezi Mungu ataiweka roho yake mahali pema peponi,” aliongeza.
Askofu Mkuu Issangya aliongeza kuwa atamkumbuka sana Dk Magufuli kama kiongozi mzalendo aliyepigania maslahi ya taifa lake kwa kutetea kwa nguvu zote rasilimali za taifa ili ziwanufaishe wananchi kwa kuwaletea maendeleo katika nyanja mbalimbali.
Rais Samia anakuwa rais wa kwanza mwanamke kuiongoza Tanzania tangu ipate uhuru, akiwa Rais wa sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu mwaka 1961.
Watangulizi wake ni pamoja na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye aliongoza kuanzia 1962 hadi 1985,Ali Hassan Mwinyi (1985-1995),Hayati Benjamin William Mkapa (1995-2005),Jakaya Mrisho Kikwete (2005-2015) na Hayati Dk John Pombe Joseph Magufuli (2015-2021)