Mabucha ya nyamapori yakosa nyama

 

 

Na Claud Gwandu, Arusha

 

MATUMAINI ya wananchi wa Tanzania kufaidi kitoweo cha wanyamapori huenda yakachukua muda mrefu kutimia baada ya wafanyabiashara waliochangamkia fursa hiyo kushindwa kuuza hata kilo moja ya nyamapori tangu Agosti, mwaka jana.

 

Biashara hiyo ya mabucha ya wanyamapori ilianzishwa kutokana na agizo la Rais John Pombe Magufuli mwaka 2019 ili wananchi wafaidi rasilimali za nchi lakini pia ikiwa ni mkakati wa kupunguza ujangili uliokuwa umeshamiri maeneo mbalimbali nchini.

 

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili unaonyesha kuwa  wafanyabiashara 46 walifanikiwa kukamilisha mlolongo mrefu na ghali wa kupata leseni na vibali vya kufanya biashara hiyo kutoka katika mamlaka zinazohusika, lakini wameshindwa kuanza kutoa huduma hiyo kwa miezi sita sasa.

 

Maeneo nane yenye mapori ya wazi waliyopangiwa kuwinda wafanyabiashara hao, ama hayana kabisa  wanyama wanaostahili kuvunwa au miundombinu si rafiki na mengine yapo kwenye umbali ambao hauwezi kuwapa faida wafanyabiashara hao.

 

Umbali wa mapori yenye wanyama wanaoweza kuvunwa unachangiwa na changamoto ya miundombinu, hasa barabara ambazo hazipitiki katika kipindi hiki ambacho mvua zinanyesha sehemu mbalimbali nchini.

 

Baadhi ya wafanyabiashara hao wenye leseni, waliozungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, wamekiri ugumu wa biashara hiyo, na kuthibitisha kuwa mpaka sasa agizo la Rais Magufuli limeshindwa kutekelezeka.

 

“Ni kweli, pamoja na mlolongo mrefu wa kupata leseni, nimeshindwa kupata hata mnyama mmoja baada ya kupangiwa kuwinda eneo la Talamai wilayani  Kiteto na Kitwai katika wilaya Simanjiro, lakini kote huko hakuna wanyama,ni hasara tu tunapata”alieleza moja wafanyabiashara Mary Methew[WU1]   mkazi wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.

 

“Gharama za uwindaji ni kubwa lakini pia maeneo tuliyopangiwa hayana kabisa wanyama,sasa tumeshawasilisha kikao chetu na tuliahidiwa tutapewa maeneo mengine kabla ya Februari 5,mwaka huu, lakini hadi leo hatujui kinachoendelea,”alisisitiza mfanyabiashara huyo.

 

Mfanyabiashara mwingine wa jijini Arusha ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema maeneo waliyopangiwa si rafiki kabisa kwao na biashara hiyo kwa kuwa hayana wanyama kabisa na yapo mbali huku barabara na miundombinu ya usafiri na usafirishaji ikiwa ni changamoto hasa katika kipindi hiki mvua zinaponyesha nchini.

 

“Tumeingia hasara kubwa sana tangu kutafuta leseni kutokana na mlolongo na masharti magumu,lakini hata baada ya kukamilisha,bado mazingira ya biashara ni magumu mno. Tunamwomba Rais Magufuli aingilie kati,’’alisema mfanyabiashara huyo na kuongeza:

 

“Hata duka la kwanza lililofunguliwa Dodoma,wanyamapori walipelekwa pale na Tawa ( Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori) kutoka pori la Kisarawe kwa kuwa pori lililo karibu na Dodoma halikuwa na mnyama hata mmoja.

 

Mapori nane ya maeneo ya wazi waliyopangiwa wafanyabiashara hao ni pamoja na Talamai(Kiteto), Kitwai (Simanjiro) yaliyopo mkoani Manyara, Ipemba Mpazi (Sikonge) mkoa wa Tabora, Simbanguru (Manyoni), Kisarawe mkoa wa Pwani,Kilwa mkoani Lindi na Ugala Ninsi yaliyopo mkoani Katavi ambapo kuna vitalu vya uwindaji.

 

Kwa upande wake William Kyaruzi ambaye aliwahi kufanya kazi lililokuwa Shirika la Wanyamapori (TAWICO) lililokuwa likiuza nyamapori kila wiki miaka ya nyuma anasema watu wanapendelea kitoweo cha wanyamapori kwa kuwa ni nyama hiyo ni dawa na haina madhara kama ilivyo nyama za Ng’ombe,Mbuzi Kondoo.

 

Aliongeza kuwa  baadhi ya nyamapori kama ya Pundamilia ni dawa kwa binadamu,hasa ute ulio katika mfupa mkuu kwenye miguu na mikono ya mbele, hivyo mahitaji ya nyama hiyo ni makubwa.

 

Katibu Mkuu wa Chama cha wenye Mabucha ya Wanyamapori Tanzania, Mchungaji Emanuel Absalom alithibitisha kuwepo kwa changamoto hizo na kusema kuwa hatua zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na kukutana na mamlaka zinazohusika.

 

“Ni kweli kuna malalamiko juu ya changamoto wanazokutana wafanyabiashara wa mabucha ya nyamapori na tulikutana na Tawa hapa Arusha mwishoni wa mwezi uliopita tukajadili kwa pamoja changamoto hizo na tukakubaliana zitashughulikiwa ndani ya wiki moja lakini bado tunasubiri,” alisema Katibu Mkuu huyo ambaye naye amefungua duka la kuuza nyamapori eneo la kwa mrombo jijini hapa.

 

Alitaja moja ya maeneo waliyokubaliana ni kuongezwa kwa maeneo ya uwindaji kutoka nane na yafikie walau 20 ili kuwawezesha wawindaji hao kupata wanyamapori kirahisi na kwa wingi, hatua itakayosaidia bei ya kitoweo hicho kuwa rahisi kwa watumiaji, kama alivyoagiza Rais Magufuli.

 

“Tuna taarifa kuwa mapendekezo ya kuongeza maeneo yameshafika mezani kwa waziri lakini baadhi ya Maofisa Wafanyamapori wa Wilaya(DGOs) tuliowasiliana nao wanasema hawajapata maagizo yoyote hivyo tunawaomba wafanyabiashara kuendelea kuwa na subira ingawa tunajua hasara wanazopata.” alisema.

 

Aliwataka wafanyabiashara wasione kuwa ni usumbufu kwa kuwa biashara hiyo ni nyeti na inahitaji udhibiti wa hali ya juu ili kukabiliana na ujangili unaoweza kujipenyeza kwa kutumia mgongo wa nia njema ya Rais Magufuli.

 

Kuhusu uanzishwaji wa mashamba ya kufuga             wanyamapori, Mchungaji Absalom alisema huo ni mpango wa muda mrefu ambao unahitaji mchakato na  uwekezaji mkubwa,na hata kama yakianzishwa leo uzalishaji wake utachukua muda mrefu.

 

“Suluhisho la kudumu la kupata kirahisi  wanyamapori kwa ajili ya kitoweo ni kuwa na mashamba ya kufuga wanyamapori, na wenzetu Afrika Kusini wamefanikiwa sana katika hilo. Lakini, kwa mujibu wa sheria, mfugaji unatakiwa kuwa na mashamba makubwa yasiyopungua hekta 2500 yakiwa na miundo mbinu kama uzio wa kuzunguka shamba lote,maji ya kutosha ambayo ni gharama,” alisisitiza Katibu Mkuu huyo wa Chama cha wenye Mabucha ya Wanyamapori Tanznaia.

 

Msimamizi wa Mabucha ya Wanyamapori wa TAWA, Gregory Kalokola alipoulizwa juu ya malalamiko hayo  alikiri kuyapokea na kwamba walikubaliana katika kikao cha pamoja cha wadau kilichofanyika Januari 27 hadi 29, mwaka huu jijini Arusha kuwa watapeleka ombi kwa waziri mwenye dhamana waongezewe maeneo ya uwindaji.

 

“Ni kweli tulikubaliana na ombi tulishawasilisha kwa Waziri mhusika. Hadi sasa tunasubiri majibu kwa kuwa kisheria ndiye mwenye dhamana,

hivyo niwaombe wenye mabucha wavute subira, kwani hatutaki kurudia makosa ya kutoa maeneo ya uwindaji kama Kitwai ambayo hakuna wanyama,”alisema Kalokola kwa njia ya simu.

 

Kalokola aliongeza kuwa maamuzi ya waziri pia yatategemea mchakato wa wataalam wa kutembelea maeneo yaliyopendekezwa ili

kujiridhisha kama wanyamapori wapo na hakuna migogoro na wadau wengine katika maeneo husika.