Wakulima wa kitunguu mang’ola walia na athari za corona, bei yaporomoka

kitunguu kikiwa kimejazwa kwenye mifuko tayari kwa kuuzwa
Moja ya mashamba ya kitunguu katika bonde la mang’ola likiwa limevunwa

 Na Seif
Mangwangi, Arusha

WAKATI
Wataalam wa tiba duniani wakiendelea na harakati za kutafuta tiba ya mlipuko wa
ugonjwa wa homa ya Mapafu maarufu kwa jina la Corona (Covid -19), athari za
ugonjwa huo zimeendelea kuonekana nchini hususani katika sekta ya Kilimo.

Wakulima
wa kitunguu katika eneo la kata ya Mang’ola lililopo wilaya ya Karatu Jijini
Arusha, wamesema bei ya kitunguu imeporomoka na kuwasababishia hasara kubwa
tofauti na matarajio yao.

Wakizungumza
na APC Blog, baadhi ya wakulima katika bonde hilo maarufu nchini kwa uzalishaji
wa vitunguu vyenye ubora wa hali ya juu katika ukanda wa Afrika Mashariki
walisema kuporomoka kwa bei kumesababishwa na athari za ugonjwa wa CORONA.

Walisema
kuwa kutokana na ubora wa kitunguu kinachozalishwa kataka bonde hilo wanunuzi
wamekuwa wakitoka katika nchi za Kenya na Uganda na ambao wamekuwa wakinunua
kwa bei ya juu tofauti na mauzo ya ndani.

Wakulima
hao walisema kuwa wanunuzi hao wamekuwa wakipeleka kitunguu chao hadi katika
nchi za ulaya na hivyo kuwanufaisha wakulima katika bonde hilo kwa bei nzuri ya
ununuzi na ambayo ilikuwa ikivutia wakulima wengi kujikita kwenye kilimo cha
zao hilo.

Given
Kessy ni mmoja wa
 wakulima katika bonde
hilo ambaye anasema kuwa tangu ugonjwa wa corona ulipoingia nchini hali ya
mauzo ya kitunguu imeshuka kwa kasi kubwa kutokana na kutegemea soko la ndani ya
nchi.

Amesema
kuwa wakulima katika bonde hilo wamepata hasara kubwa kutokana na mauzo ya
kitunguu kuwa ya bei ya chini ambayo hailingani na hali halisi ya gharama
ambazo wamekuwa wakizitumia tangu kutayarisha shamba hadi kuvuna.

“ Mimi
nimelima ekari moja ambapo hadi hivi sasa nimeshatumia si chini ya Tsh Milioni
6, pesa ambayo nilitegemea kuipata na faida yake baada ya kuuza kitunguu kwa
faida, lakini bei zilizopo sokoni hivi sasa zinatisha, ni ndogo na haziwezi
kurejesha gharama nilizotumia kulimia,”amesema Kessy.

Kwa upande
wake Mkulima mwingine Emmanuel Laizer anasema kuwa tangu kulipuka kwa ugonjwa
wa Corona, wakulima wa vitunguu bonde la Mang’ola wamekuwa wakipata hasara
kutokana na gharama kubwa wanayoitumia kukuzia zao hilo.

“Mimi
nimekuwa nikilima maeneo mbalimbali nchini, kama hapa Mang’ola na Singida, ila
gharama za hapa ni kubwa sana kulinganisha na gharama za Singida, kitunguu cha
hapa ni kizuri sana na kwa kawaida bei yake pia ni ya ghali, ila baada ya
ugonjwa wa Corona kuibuka hali imekuwa tofauti, tumekuwa tukipata hasara tu
badala ya faida,”alisema.

Alisema
baadhi ya wakulima wakubwa na wenye uwezo wamekuwa
wakilazimika kuvuna vitunguu vyao na
kuvihifadhi kwa muda katika  maghala (store)
kutokana na tatizo hilo la kushuka sana kwa bei  na kukosekana kwa wanunuzi wa vitunguu hivyo
.

Laizer
aliiomba Serikali kuangalia namna ya kuwapatia masoko mengine nje ya nchi mbali
ya Kenya na Uganda ili waweze kufidia gharama ambazo wamekuwa wakiingia wakati
wa kulima zao hilo lakini pia kufanya mawasiliano na viongozi wa Kenya ili
wanunuzi wa zao hilo waruhusiwe kuingia nchini kama mwanzo.

Kwa mujibu
wa Laizer, bei ya gunia moja la kitunguu maarufu kama neti ya Magufuli
iliyokuwa inauzwa Tsh 100,000 hadi 200,000 imeshuka na hivi sasa inauzwa kati
ya Tsh 30,000 hadi 50,000 na wakati mwingine pamoja na kuwepo kwa bei hizo bado wanunuzi wanapatikana kwa tabu.