Afisa Viwango Mkuu kutoka Shirika
la Viwango Tanzania (TBS),Bw.Nickonia Mwabuka akizungumza na waandishi
wa habari leo Makao Makuu ya Shirika hilo Jijini Dar es Salaam
Wafanyabiashara na wazalishaji wa
bidhaa nchini wametakiwa kushiriki katika shindano la utoaji tuzo bora
kwa makampuni ya uzalishaji na watoa huduma itakayofanyika Machi, mwaka
2021 nchini Msumbiji katika mkutano wa mwaka unaoshughulikia vikwazo
katika biashara kwenye Jumuiya ya SADC (SADCTBT-Cooperation Structures).
Akizungumza na wandishi wa habari
Jijini Dar es Salaam, Afisa Viwango Mkuu kutoka Shirika la Viwango
Tanzania (TBS),Bw.Nickonia Mwabuka amesema tuzo hizo ni kuangalia bidhaa
zetu zinakidhi ubora katika utengenezaji na utumiaji kwaajili ya
wananchi na biashara pamoja na kukuza uchumi kwa jumuiya ya SADC.
“Tunawaomba wadau wote katika
uzalishaji na kutoa huduma kutumia nafasi hii ya kushindana iliyotolewa
na SADC, kujaza fomu husika kwa kuangalia vigezo vilivyowekwa na kutuma
TBS kwa mtandao uliowekwa, kama upo karibu unaweza kuleta mwisho ni
Jumatano saa 10 jioni”.Amesema Bw.Mwabuka.
Aidha Bw.Mwabuka amesema makundi
yote yatakayo shiriki watajaza fomu maalumu iliyoandaliwa ambayo ipo
kwenye tovuti ya TBS- www.tbs.go.tz, ZBS- www.zbs.go.tz na kuirejesha
kwa kutumia email qualityawards@tbs.go.tz Novemba 25 mwaka huu.
Pamoja na hayo Bw.Mwabuka amesema mshindi wa kwanza katika kila kundi atapewa cheti cha ushindani na kombe.
“Washindi hao pia watashiriki
katika mkutano wa SADCTBT utakaofanyika Machi 2021 Maputo nchini
Msumbiji ambaye ndiye atakuwa Mwenyekiti wa SADC”. Amesema Bw.Mwabuka.
Hata hivyo amesema kuwa faida ya
kushiriki katika mashindano hayo ni pamoja na kufanya bidhaa na huduma
zetu kwa ujumla kujulikana katika soko la SADC.
Sambamba na hayo amesema kuwa
makundi ambayo yatashiriki ambayo ni kundi la wajasiriamali chini ya
watu 100,Wazalishaji wakati ma wakubwa zaidi ya wafanyakazi 100,mtu
binafsi anayezalisha/kutoa huduma inayokidhi ubora.
Amesema utoaji wa tuzo kwa
makampuni ya uzalishaji na watoa huduma ni utaratibu ambao hufanyika
kila mwaka kwa wanachama wa SADC kwa lengo la kutambua mchango wa
matumizi ya viwango katika kukidhi ubora wa bidhaa na huduma kwa jamii
ya SADC.
Tuzo ya hizo zimeandaliwa na
Shirika la Viwango TBS na Shirika la Viwango Zanzibar (ZBS)
wakishirikiana na taasisi za sekta binafsi bara na visiwani.