Pichani Ni Kaimu Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania Bwana Imani Sichalwe akiwa na viongozi wa Umoja wa wabeba Nyama Kwenye bodaboda Machinjio ya Vingunguti.
Na.Vero Ignatus.
Bodi ya nyama nchini imejipanga kuandaa utaratibu mzuri wa usajili wa wabeba nyama kwa njia ya pikipiki(bodaboda), kutoka katika machinjio hadi kwenye mabucha mbalimbali ya nyama Nchini.
Hayo yamesemwa na Kaimu msajili wa bodi ya nyama nchini Imani Sichalwe, wakati akizungumza na Viongozi wa Umoja wa wasafirishaji wa nyama kwa kutumia pikipiki (bodaboda), wanaofanya shughuli zao kwenye machinjio ya vingunguti Dar-es-Salaam.
Sichalwe amesema kuwa kwa mujibu wa taratibu na sheria, hairuhusiwi kufanya biashara ya nyama, kama haujasajiliwa na bodi ya nyama,na katika usajili huo bodi ya nyama imekuwa ikisajili magari ya kubebea nyama ,ila wabebaji wa nyama kwa njia ya pikipiki yaani bodaboda ndio waliokuwa hawajasajiliwa ,licha ya kuonekana wakisafirisha nyama.
Amesema kwa mujibu wa kanuni zilizopo za usajili na ukaguzi , zinayohusu biashara ya nyama hairuhusiwi kusafirisha nyama kwa njia ya bodaboda,Kwa Muktadha huo bodi ya nyama ikaona ni vyema kuja na mpango wa kuwasajili, ili waweze kutambulika na kupewa utaratibu mzuri,wa kubeba nyama kwasababu nyama ni kitoweo muhimu sana kwa binadamu na ndio Maana zikawepo kanuni mbalimbali,Miongozo na sheria lengo likiwa ni kuongeza ubora na usalama wa nyama Nchini.
Sichalwe amesema kiutaratibu nyama hairuhusi kubebwa kwenye Vifaa vyovyote vya plastiki, isipokuwa kwenye vyombo vya alminiamu ,au vile vyombo ambavyo ni rahisi kusafishika na havitoi kutu,kwa hivyo utaratibu unaotumika kubeba nyama kwenye bodaboda ni kinyume na utaratibu.
”Kwakuwa hutumika mifuko ya salfeti kuwekea nyama na utakuta mifuko yenyewe ni michafu, kisha wanatumbukiza nyama kwenye madeli ya plastiki ,ambayo sio rahisi kusafishika jambo linaloharibu ubora na na kuhatarisha usalama wa mtumiaji”Alisema Sichalwe.
Aidha miongoni mwa majukumu ya bodi ya nyama nchini ni Kuendeleza sekta ya nyama, hivyo bodi hiyo imeona ni vyema kutumia utaratibu wa kukutana na viongozi wa umoja wa wabeba nyama ,kwa bodaboda machinjio ya vingunguti na kuwapa elimu,Pamoja na kuwaelezea juu ya uwepo wa fursa za ufanyaji wa biashara ya kusafirisha nyama kwa bodaboda, kwa mujibu wa sheria na kanuni na miongozo inayohusiana na utaratibu mzuri wa ubebaji nyama kama sheria na kanuni, zinavyoelekeza ili kuendeleza falsafa ya bodi isemayo nyama bora na salama kwa wote.
Akiongelea kifaa hicho maalumu ambacho kitakuwa kinatumika kubebea nyama,kitakachokuwa kinafungwa kwenye bodaboda Imani Sichalwe ,amesema kitakuwa hakiwezi kuruhusu joto wala baridi kuingia isipokuwa ukiweka nyama joto ambalo lipo mule ndani ya hicho kifaa maalumu, linabaki vile vile hivyo, kinachotakiwa hapo ni kuweka barafu kwasababu nyama inatakiwa iwe kwenye ubaridi kisha unafunga ,hivyo kufanya nyama iendelee kuwa safi na salama tofauti na wanavyosafirisha sasa.
”Mvua ikinyesha inanyeshea nyama,wakipita kwenye maji machafu yanamwagikia,wakipita kwenye vumbi linaingia kwenye nyama jambo ambalo linasababisha nyama kupoteza ubora na kuhatarisha afya ya mlaji”Alisema
Akizungumza kwa niaba ya wenzake Mwenyekiti wa Umoja wa wabeba nyama kwa bodaboda machinjio ya vingunguti Godfrey Jastini ,ameshukuru hatua ya bodi kuja na mkakati wa kuwatambua kwa mujibu wa sheria ,na kuwasajili ili wabebe nyama kwa utaratibu mzuri jambo litakalopelekea kuongeza usalama wa nyama kwa mtumiaji ,na kuomba mpango huu ufanye haraka ili vijana waweze kufanya biashara ,hii kwa uhuru na kufuata sheria na kanuni za usafirishaji wa nyama Nchini.
‘’Nitakwenda kufanya kikao na wanachama wangu kuwaeleza juu bodi ya nyama nchini,na ni ukweli usiopingika vijana wengi tumehamasika kufanya biashara hii ya ubebaji wa nyama kwa njia ya bodaboda kutoka kwenye machinjio japo tunakutana na vikwazo vingi kwasababu hatujasajiliwa kwa mujibu wa sheria, na hata ubebaji baadhi yetu hatuzingatii usafi na usalama, ukizingatia vyombo tunavyobebea sio salama kwakuwa havisafishiki kwa urahisi,kwa hiyo tunashukuru sana kwa Elimu nzuri ya namna bora ya ubebaji wa nyama kwenye bodaboda na kuambiwa uwepo wa vifaa maalumu vya kubebea nyama kwenye bodaboda kutoka kwenye machinjio hadi kwa mabucha ya kuuzia nyama’’alisema Godfrey Jastini Mwenyekiti wa umoja wa wabeba nyama kwenye bodaboda machinjio ya Vingunguti.
Mpango huu wa usajili wa madereva wa bodaboda wanaobeba nyama ,kutoka kwenye machinjio mbalimbali kwenda kwenye mabucha, utafanyika nchi nzima na utasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza wigo kwa vijana kujiajiri, katika ubebaji wa nyama kwenye bodaboda, ikiwa na utekelezaji wa kauli mbiu ya bodi ya nyam,a inayosema ‘’Nyama bora na salama kwa wote’’ Jambo litakalosaidia kuchochea kasi ya maendeleo ya sekta ya nyama Nchini.