Mwandishi wa habari na Mmiliki wa Mbeya Yetu Online TV Joseph Mwaisango |
Na Joachim Nyambo,Mbeya.
WANAHABARI Mkoani Mbeya wamesema wanayo imani kubwa ya utendaji kazi wa kipindi cha pili cha Serikali ya awamu ya tano chini ya Dk John Magufuli kwa kuwa sasa watendaji wengi wanatambua nini kiongozi huyo anahitaji kwenye utumishi wake kwa watanzania.
Wanahabari hao wamesema wanaamini tumbua tumbua ya mawaziri na watendaji wengine iliyoonekana katika awamu iliyopita hususani miaka ya mwanzoni mwa utawala huo ulitokana na wateule wengi kutotambua nia ya dhati ya Dk Magufuli ya kuwatumikia watanzania katika ari ya uwazi,kujituma na uwajibikaji wa kweli.
Mmoja wa wanahabari hao,Hines Thobias alisema matarajio ya watanzania ni kuona mawaziri na wateule wengine watakwenda kwa kasi anayoitaka Magufuli katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Hines alisema pia baada ya wananchi kutambua uchapa kazi wa Magufuli ni wazi kuwa wataongeza kasi ya kujituma katika kazi hatua aliyosema itawezesha zaidi kuchochea kwa kukua kwa uchumi wa Tanzania na taifa kupata sifa zidi kwa kupiga hatua nzuri zaidi kiuchumi.
Mwanahabari Samuel Ndoni alisema matarajio ya wanaMbeya kupitia wawamu ya pili ya Dk Magufuli ni kuona mkoa huo unakuwa lango kuu la kiuchumi katika nchi za kusini mwa Afrika(SADC) kwa kuwekewa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo miundombinu ya barabara,reli ya Tazara,Bandari za ziwa Nyasa,Uwanja wa ndege wa Songwe na Bandari kavu inayotarajiwa kujengwa Inyara Mbeya vijijini.
“Pia kwakuwa mkoa wa Mbeya ni miongoni mwa mikoa inayozalisha kwa wingi chakula nchini kupitia kilimo natarajia kuwepo kwa viwanda vya msingi na vikubwakwenye maeneo yanayozalisha mazao ili kuyaongezea thamani na kuleta tija kwa wakulima wakubwa na wadogo.”
Kwa upande wake Hosea Cheyo,alisema matarajio ya Tanzania kupaa zaidi kimaendeleo ni makubwa kwakuwa dalili njema zilianza kuonekana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita lakini akasema ili kuwezesha hilo ni muhimu mpango wa Mtandao wa usafiri na usafirishaji hususani wa Barabara kuunganishwa kuendelea kupewa mkazo.
Joseph Mwaisango alisema sambamba na mipango mingine,watanzaanzia wanayo matumaini makubwa ya Serikali kuendelea kuboresha sekta ya elimu ya msingi sambamba na miundpombinu ya usafiri hususani barabara kutokana na umuhimu wake katika kusafirisha mazo ya wakulima kutoka mashambani hadi yaliko masoko.
“Lakini pia katika siku za hivi karibuni kumekuwa na mchango mkubwa wa mitandao ya kijamii zikiwemo luninga zaa mitandaoni.Ni muhimu Serikali ikipa uangalizi wa kipekee eneo hili ili litoe mchango chanya kwenye maendeleo ya taifa letu.Iruhusu mitandao iliyo makini na hiyo ikiwezekane iweze kupewa ruzuku ili iweze kujiendesha na pia gharama za kulipia leseni kwa wamiliki wanaoonekana kufuata maelekezo yanayotakiwa na TCRA basi zipunguzwe.” Alisema Mwaisango.
Naye Felister Richard alisema wanatasnia ya habari nchini wanayo matarajio makubwa kwa awamu ya pili ya Dk Magufuli kutupia jicho katika maslahi na mazingira wanayofanyia kazi.
“Tunapenda tuone wanahabari wanalipwa mishahara na waajiri kulingana na elimu zao kwa kuzingatia kima cha chini cha mshahara,maslahi kwa wanaowaita wanajitolea lakini p;ia kuwalipa wafanyakazi muda wa ziada na kuwalipia mifuko ya hifadhi za jamii.Lakini pia tungependa kuona kwa wanahabari walioitumikia tasnia hii maisha yao baada ya kazi hiyo yanaandaliwaje kwakuwa na wao mchango wao ni mkubwa katika maendeleo ya taifa lao.” Alisema Felister.