Gari za kubeba watalii zikiwa zimebaki nje ya moja ya hoteli za kitalii zilizoko katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti baada ya kuteremsha watalii |
Na Mwandishi Wetu, Arusha
UKOSEFU wa ajira katika sekta ya
utalii nchini kumeelezwa kusababisha baadhi ya wafanyakazi waliokuwa
wakifanyakazi katika kampuni za utalii pamoja na kuhudumu kwenye hoteli
mbalimbali za kitalii Jijini Arusha kutelekeza familia.
Akizungumza kwa masharti ya
kutotajwa jina lake, mmoja wa madereva wa utalii jijini Arusha amesema kuwa
tangu kulipolipuka kwa ugonjwa wa Corona nchini, wafanyakazi katika kampuni za
utalii walipunguzwa na zingine zilifunga.
Alisema kutokana na ukata
uliowakumba kwa zaidi ya miezi kumi sasa, amelazimika kumrudisha mke kwa wazazi
wake huku watoto akiwapeleka kijijini kwa wazazi wake baada ya kukosa fedha za
kujikimu na kuhudumia familia.
Kutokana na ukata huo, anasema
amelazimika kufanya kazi za kusaidia fundi kwenye sekta ya ujenzi wa nyumba na
kupata fedha kidogo ambayo imekuwa ikimsaidia kupata mlo lakini pia kulipia
kodi ya pango la nyumba katika chumba kimoja alichokipanga maeneo ya Kwa
mromboo nje kidogo ya jiji la Arusha.
“Ndugu yangu madhara ya Corona ni
makubwa sana, sisi watu wa utalii tulifikiri ni masihara lakini ukweli hali ni
mbaya sana, nimelazimika kumrudisha mke wangu kwao kwa sababu kwa kweli sina
kipato cha kuendelea kumtunza kwa sasa na watoto nimewapeleka kijijini kwa
wazazi wangu,”anasema.
Kwa upande wake Edward Selasini,
mkazi wa Arusha ambaye amekuwa akijishughulisha na shughuli za utalii anasema
kuwa sekta ya utalii imepata pigo kubwa sana baada ya wengi wa wafanyakazi
waliokuwa wameajiriwa kujikuta wakilazimika kufanyakazi ambazo hawajawahi
kuzifanya hapo mwazo ili kujikimu kimaisha.
“Baada ya utalii kuanguka ninao
rafiki zangu wengi sana wamejikuta wakianza kutafuta kazi pasipokufanikiwa na
wengine wamejiingiza kwenye kilimo na wengine wameanza kufuga mifugo
midogo midogo kama kuku na kuuza,”anasema.
Anasema kutokana na hali ya maisha kuwa mbaya kwa
wafanyakazi walikuwa katika sekta ya utalii, anaiomba Serikali kuangalia namna
ya kuweza kusaidia sekta hiyo ikiwemo kutoa mikopo itakayowawezesha kufanya
biashara na kupata kipato cha kujikimu.
…………………………………………………………………………………………………………………………………………………