Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini na Madhehebu mbalimbali Mkoa wa Singida,(aliyesimama)Hamis Muhamed Kisuke akiongoza kikao ambapo walizungumzia hali ya amani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu na kuja na maazimo saba. (Picha na Rose Nyangasa).
Singida Dkt. Rehema Nchimbi akizungumza
na Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini na
Madhehebu mbalimbali Mkoa wa Singida ambapo
ameipongeza Kamati hiyo kwa kuamua
kuhamasisha amani na utulivu kwenye
kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu (Picha na Rose Nyangasa)
Wajumbe wa Kamati ya Amani Mkoa wa Singida wakimsikiliza kwa makini Kamanda wa Polisi wa MKoa wa Singida, Sweetbert Njewike (hayupo pichani) wakati akielezea majukumu ya jeshi hilo kwenye siku ya upigaji kura Oktoba 28, mwaka huu. (Picha na Rose Nyangasa).
Kamanda wa Polisi wa MKoa wa Singida, Sweetbert Njewike majukumu ya jeshi hilo kwenye siku ya upigaji kura Oktoba 28, mwaka huu. (Picha na Rose Nyangasa).
John Mapepele na Rose Nyangasa, Singida
Kamati ya Amani
na Dini mbalimbali Mkoa wa Singida
inayojumuisha viongozi wa madhehebu na
dini zote imetoa tamko lenye maazimio
saba kuelekea Uchaguzi Mkuu
utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu huku
ikiwaomba waumini wao kumtanguliza Mungu na Serikali kusimamia
amani na utulivu ili kuwapata viongozi bora watakaoingoza nchi katika miaka mitano ijayo 2020 hadi 2025.
Akisoma
maazimio hayo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo
Shehe, Hamis Muhamed Kisuke amesema miongoni mwa maazimio hayo ni kuwaomba waumini wao kutenga siku tatu
kuanzia Ijumaa hadi Jumapili ya juma hili kwa ajili ya kufunga na kuomba ili kuombea uchaguzi upite kwa
amani na usalama.
Maazimio mengine yaliyofikiwa kwenye kikao hicho ni pamoja
na viongozi wa dini katika kipindi hiki
kudumisha Amani, kutotumika kwenye majukwaani ya siasa kushabikia viongozi wa vyama vya siasa, kuhubiri Amani,
kuhimiza waumini wao kushiriki kupiga
kura na kuhimiza kufuata na kutii sheria za
nchi ambapo pia wamesisitiza
kuviacha vyombo halali vilivyopewa
dhamana ya kusimamia uchaguzi huo vifanye kazi yake.
Mwakilishi wa
dini ya Kiislam (Baraza la Kiislam Tanzania) katika Mkoa wa Singida Shehe, Issa Nassor amesema
Amani ikitoweka watakaoumia
zaidi ni watoto, wanawake,
wajawazito, wazee na watu wenye mahitaji
maalum kwa kuwa hawana uwezo wa
kukimbia na kujitetea.
Aidha, wamewataka wazazi na walezi wa kila familia kuwaasa
vijana kujiepusha na kushawishiwa na watu wanaoitakia mabaya
nchi ya Tanzania ambapo ameongeza
kwamba baada ya kupiga kura
vijana warejee nyumbani kwa
kuwa tayari Serikali imeshaweka
vyombo maalum kwa ajili kuhesabu na kutangaza matokeo hayo.
“Historia
inaonyesha kuwa nchi zote duniani zilizopoteza amani ni nchi ambazo walilewa
amani, vilevile tukumbuke kupata amani ni mchakao wakati kuvunja amani
ni jambo rahisi kabisa. Nawaomba
watanzania wenzangu kutumia vipande
vyetu vya kupigia kura kuwachagua Viongozi bora” aliongeza Shehe, Nassor
Mwakilishi kwa
upande wa wakristo, Askofu wa Kanisa la TAG mkoani Singida, Gasper Mdimi
amesema amani ya nchi ni jambo nyeti ambalo linatakiwa
kuchukuliwa kwa uangalifu mkubwa
kwa kuwa lina athari pana
kuanzia kwenye ngazi ya
kaya hadi taifa kwa ujumla na kwamba
Bibilia imefafanua kuwa chanzo
cha Amani ni Mungu mwenyewe, Haki na Watu wanaomcha Mungu.
Amefafanua kuwa vitabu vyote
vitakatifu vinasisitiza
kutafuta kuwa na amani
na watu wote ambapo na kwamba
watanzania wanatakiwa kupendana katika kipindi hiki bila kuangalia
vyama vyao vya Siasa
na kuiombea nchi yao ipate
viongozi ambao watailinda amani.
Pia
amesema wakati wananchi wanakwenda katika siku za mwisho wa kuhitimisha zoezi la
kuwachagua viongozi ni muhimu
kuzingatia kuacha kuongea maneno
ambayo yatasababisha machafuko na
uvunjifu wa amani.
Mwakilishi wa
Mhashamu Baba Askofu wa Jimbo Katoliki la Singida, Padre Padri Elia
Mnyakanka amesema Uongozi Bora ni tunu na zao
la amani na kwamba ili kuwa na maendeleo na ustawi kuanzia ngazi ya familia na taifa ni muhimu
kwa wananchi kutafakari kwa kina na kuwachagua viongozi wanaoweza kuilinda
amani.
Akitoa mfano
amesema katika taifa la Israel uongozi bora ulikuwa ni nyenzo ya
kuwafikisha kwenye nchi ya ahadi kupitia
manabii mbalimbali ambapo kwa kufanya hivyo amani ilipatikana.
Amesema viongozi wa dini wanapaswa kuwapa elimu ya uraia waumini wao ili kuwapa
uwezo wa kuwachagua wagombea makini kupitia ilani zao ambapo amesisitiza kwamba uchaguzi wa haki na amani ndiyo njia
pekee ya kujitawala na kuleta amani katika nchi.
Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Singida, Sweetbert
Njewike amesema kwenye kipindi hiki cha uchaguzi majukumu yao ni pamoja na
kutunza na kudumisha Amani, kusimamia utekelezaji wa sheria, kuzuia na
kubaini makosa ya jinai, kuwakamata wahalifu wanaohatarisha amani na
kuwafikisha katika vyombo vya sheria, kulinda
mali za raia, kutoa ulinzi kwa maafisa na vituo, pia kuhakikisha hakuna
mtu anaye watishia wapiga kura na kuhakikisha usalama wa vifaa vya kupigia
kura.
Mkuu wa Mkoa
Singida Dkt.Rehema Nchimbi amewashukuru viongozi hao kwa kuandaa mkutano huu ambao umelenga kudumisha amani na
kuwahimiza wananchi washiriki kikamilifu kupiga kura ili kuwa chagua viongozi bora.
Aidha Dkt.Nchimbi
amewataka Viongozi wa Dini kutotumika kuharibu amani na mshikamano ambao upo kwa kipindi kirefu sasa hapa nchini
kutokana na kazi nzuri ya kusimamia
amani hiyo iliyofanywa na Serikali.