Mkuu wa wilaya ya Kilolo Asia Abdallah katikati akiwa na mgombea ubunge Kilolo Justin Nyamoga kushoto na mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kilolo Kilian Mnyenzi mara baada ya mkutano wa kampeni kata ya Ilula .
………………………………………………………..
MGOMBEA ubunge wa jimbo la Kilolo kupitia chama cha mapinduzi (CCM) Justin Nyamoga amewataka wananchi wa jimbo hilo kutofanya majaribio ya kuchagua viongozi wakati wa uchaguzi mkuu utakaofanyika octoba 28 mwaka huu.Mwandishi Francis Godwin anaripoti kutoka Kilolo
Nyamoga ametoa ushauri huo jana wakati wa uzinduzi wa kampeni za udiwani kata ya Ilula kuwa lazima wananchi kuwa makini katika kuchagua na kuacha kuacha kuchagua kwa ushabiki na badala yake kuwachagua wagombea baada ya kusikiliza sera na wale wenye ilani ya uchaguzi badala ya kuchagua wagombea wanaopanda jukwaani kunadi kejeli na matusi dhidi ya serikali .
” Tambueni mnapo mpigia diwani ,mbunge na Rais kura hizo mmewakopesha na wanatakiwa kuwalipa maendeleo ndani ya kipindi cha miaka mitano hivyo umakini unahitajika wakati wa kupiga kura hakikisheni wote tunaokuja mbele yenu katika majukwaa ya kampeni tuwaelezeni nini tutawafanyia mkituchagua sio kuleta porojo zisizo na tija” alisema Nyamoga
Kuwa kwa upande wa wagombea wa CCM kila wanapopanda jukwaani wamekuwa na ilani ya uchaguzi ambayo imebeba mambo mbali mbali ambayo iwapo wananchi watakopesha kura zao siku ya uchaguzi mkuu basi mambo hayo ya kimaendeleo yaliyopo kwenye ilani yatakwenda kutekelezwa na kupitia ilani hiyo ni rahisi kwa wananchi kumbana mwakilishi wao iwapo atashindwa kutekeleza .
Kwani alisema ndani ya ilani ya uchaguzi ya CCM imeeleza wazi kwa mikaka mitano itafanya nini katika afya ,miundo mbinu ya maji ,barabara ,umeme ,kilimo na mambo mengi ya kimaendeleo ambayo ni hitaji kubwa la wananchi tofauti na wapinzani ambao badala ya kuja na ilani ama karatasi lenye vipaumbele vyao wao wanapanda jukwaani na mambo ya porojo yasiyo na tija kwa maendeleo ya wananchi .
Nyamoga alisema wananchi wa jimbo la Kilolo wanahitaji maendeleo na wanatamani kupata mbunge ,diwani na Rais mpenda maendeleo na sio kumpata mtu wa kuwahubiria chuki na porojo .
Alisema kwa kuwa unapomkopesha mtu mkopo unategemea kulipwa ni lazima kumkopesha yule ambae ni mlipaji mzuri na sio kumpa mkopo mtu ambae mkorofi katika urejeshaji mkopo na kudai kuwa CCM ni wakopaji maaminifu zaidi maana wananchi walikopesha kura zao mwaka 2015 na hadi sasa hakuna mkopo ambao haujalipwa maana wameweza kulipa na chenji imebaki hivyo ni matumani ya CCM kuona wanaongezewa mkopo mwingine wa kura octoba 28 ili waweze kuutumia kuleta maendeleo kwa miaka mitano .
Nyamoga akipokea picha zawadi ya picha yake iliyochorwa na kijana wa Ilula
Mgombea huyo alisema kura ambazo waliikopesha CCM mwaka 2015 zimeweza kuwalipa wananchi maji Ilula pia umeme hadi sasa ni vijiji 21 pekee ndivyo vimebaki pia vituo vya afya vitano vimejengwa katika wilaya ya Kilolo .
Kwa upande wake mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa (NEC) Terresia Mtewele ambae ndie alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo alisema kuwa bado matumani makubwa ya wananchi Tanzania yapo ndani ya CCM kutokana na kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Magufuli .
Mtewele alisema kuwa pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na wapinzani kubeza miradi mikubwa iliyotekelezwa na serikali ya CCM ila miradi hiyo imekuwa na faida kubwa katika ukuaji wa uchumi wa Taifa na hata wananchi wa vijijini wananufaika na ukuaji wa uchumi hivyo ni wakati mzuri wa wananchi kuwabeza wapinzani kwa kuwanyima kura siku ya uchaguzi mkuu .
Huku mkuu wa wilaya ya Kilolo Asia Abdalah akisalimia katika mkutano huo alisema kuwa kwa upande wa serikali imeendelea kutatua kero mbali mbali za wananchi wa wilaya ya Kilolo na kero kubwa ya maji katika mji wa Ilula imetatuliwa hivyo wananchi wenye kero wasisite kuitoa kwa viongozi wa serikali ili ifanyiwe kazi.
Mkuu huyo wa wilaya alisema viongozi wa serikali ni wasimamizi wakuu wa miradi ya kimaendeleo na kwa upande wake amefurahishwa na mwaliko wa CCM katika mkutano huo kwani yeye vyama vyote vya siasa ni vyake na akialikwa anafika maana jukumu lake ni ulinzi na usalama na kuona uchaguzi unafanyika katika hali ya amani na utulivu katika wilaya hiyo ya Kilolo.
Aidha Asia alisema amefanikiwa kufanya ziara mbali mbali katika wilaya ya Kilolo likiwemo eneo la Ilula na kusikiliza kero za wananchi pamoja na kuzitatua ikiwemo kero ya maji iliyokuwa ikiwatesa wanawake wa mji wa Ilula ambapo sasa ndoa zao zipo salama zaidi na hakuna mwanamke anayepigwa kwa kuchelewa kutafuta maji.