Msemaji wa klabu ya Simba SC, Haji Manara amechukizwa na kitendo cha baadhi ya mashabiki wa Yanga kumpiga na kumchania jezi shabiki aliyeva jezi ya Simba katika kilele cha Wiki ya Mwananchi siku ya Jumapili katika uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Haji Manara amesema Yanga wanatakiwa kuwaelimisha mashabiki wao kwani kitendo walichokifanya baadhi ya mashabiki wao si ugwana, soka ni upendo nasio uadui.
“Viongozi wa Yanga waelimisheni washabiki wenu, huu upumbavu ukiachwa uendelee kuna siku yatakuja kutokea maafa uwanjani.
“Soka siyo uadui, soka ni upendo na sisi ni watani wa jadi na ndio maana washabiki wenu walikuja katika sherehe yetu (Simba Day) na hawakupata bughudha yoyote, kumpiga shabiki wetu ni zaidi ya upumbavu, achana na kumchania jezi yake. Hii sio sawa na ni ushamba wa kindezi” alisema Manara.