Watumishi wa afya wametakiwa kusimamia maadili wakati wa kumuhudumia mgonjwa

 

Na WAMJW- Bombo, Tanga

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi ameagiza Watumishi wa Afya kusimamia maadili na kujishusha pindi wanapotoa huduma, ili kuondoa malalamiko yanayotolewa na wananchi wanaokuja kupata huduma. 

Prof. Makubi ametoa rai hiyo wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga – Bombo, ikiwa ni sehemu ya maboresho ya huduma za Afya kwa wananchi. 

“Nitoe wito kwa Watumishi wote katika maeneo ya kutoa huduma hapa Hospitali, turudi katika maadili yetu na kujishusha wakati wa kumuhudumia mgonjwa, huduma kwa wagonjwa ianzie  getini mgonjwa anapoingia mpaka anapotoka” alisema Prof. Makubi. 

Kwa upande mwingine, Prof. Makubi ametoa wito kwa Watumishi wote wanaotoa huduma za afya kudumisha umoja na ushirikiano baina yao katika maeneo ya kazi, jambo litalosaidia kuboresha huduma za Afya kwa wananchi wenye uhitaji. 

“Niwaombe sana kada zote katika maeneo ya kutoa huduma za Afya  muungane muwe kitu kimoja baina yenu, ili kuboresha utoaji huduma, wengine wakiona watafuata mfano wenu ” alisema Prof. Makubi. 

Aidha, Prof. Makubi kwa kiasi kikubwa ameridhishwa na hali ya utoaji huduma katika kitengo cha dharura na mapokezi, huku akisisitiza ni vyema Idara nyingine kuiga mfano mzuri ili kuboresha huduma za Afya kwa wananchi. 

Mbali na hayo, Prof. Makubi ameeleza kwa Watoa huduma wote kutoa mrejesho kwa wagonjwa pindi wanapokuja kupata huduma ili kuondoa mkanganyiko unaoweza kujitokeza bila sababu ya msingi. 

Prof Makubi ambaye pia alipata nafasi ya kuwaona wagonjwa waliolazwa na kushaurina na Madaktari na wauguzi katika kutoa huduma za tiba, alibaini changamoto kwa wagonjwa kuchelewa kuona wanapolazwa ambapo ameagiza muda ya wagonjwa kuonwa katika vituo afya uwe mfupi kwa kupunguza ucheleweshaji katika hatua zote anazopita mgonjwa. 

Naye, Mkurugenzi wa Tiba Wizara ya Afya Dkt. Grace Maghembe  ametoa wito kwa viongozi kujenga tabia ya kusikiliza na kutatua kero za Watumishi wao wanaowaongoza, jambo litalokuwa chachu ya kutoa huduma bora kwa wananchi mwenye uhitaji…