Na Ahmed Mahmoud Arusha
Katibu Tawala wa mkoa wa Arusha Richard Kwitega amesema sensa ya
takwimu za Kilimo mifugo na Uvuvi itakayofanyika kuanzia mwezi ujao
taarifa itakazokusanywa itaonyesha hali halisi ya sekta ya kilimo
nchini na kuiwezesha serikali kupanga sera mipango kuimarisha na
kuboresha hali za wananchi.
Kwitega ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya
wadadisi wa sensa ya kilimo mifugo na uvuvi ya mwaka 2019/20 kutoka
mikoa ya kanda ya kaskazini yalioandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu
inayofanyika jijini Arusha.
Alisema kuwa kwa ujumla umuhimu wa kilimo unafahamika na takwimu hizo
zitaonyesha jinsi sekta hiyo inavyochangia katika pato la taifa kwani
mwaka 2019 sekta hiyo imechangia pato la taifa kwa asilimia 26.6 huku
upande wa mauzo ya nje asilimia 24.3 ya fedha za kigeni
ilipatikana.
Aidha alibainisha kuwa tafsiri ya takwimu hizo kuwa mwaka huo wakulima
tulizalisha zaidi tukavuna zaidi na kuuza zaidi huku wafugaji walifuga
zaidi wakauza zaidi na wakazalisha zaidi hivyo hatuna budi kujivunia
mchango wetu kwa sababu tunachangia katika kukuza maendeleo
tunayoyaona sasa.
Alisema kuwa Wakati tukielekea kwenye sensa ya kilimo Mifugo na Uvuvi
ya mwaka 2019/20 hatuna budi kuwakumbusha na kusisitiza kuwa mafanikio
niliyoyataja hapo awali yanatokana na matumizi ya matokeo ya sensa ya
mwaka 2007/8 ambayo ilifanyika kwa ufanisi mkubwa kwa kuonyesha maeneo
tuliofanikiwa na kupiga hatua kubwa maeneo yaliosogea kidogo na yenye
changamoto nyingi ambayo hayakupiga hatua kabisa pamoja na mipango na
sera tulizotumia kufanikiwa.
“Kama alivyoeleza awali mwakilishi wa Mtakwimu mkuu wa serikali
mafunzo haya yatakuwa na sehemu mbili za nadharia na vitendo itahusu
kujaza dodoso la wakulima wadogo na wakubwa pia dodoso la mashamba
makubwa la jamii mbinu za udadisi na kutumia teknolojia mpya katika
kukusanya Takwimu kwa matumizi ya vishikwambi kwa kufuta sheria ya
Takwimu muwe makini wa kuchukuwa taarifa sahihi”
Aliwataka kuanzia sasa tunapoitisha vikao vyetu kuhakikisha kuwa
ujumbe wa sensa uwe wa kudumu katika mikutano yetu na wananchi
tuelimishe na kuhimiza kutoa ushirikiano kwa wadadisi wakati wote wa
zoezi hili linapofanyika na kwa upande wa wananchi wajibu wao mkubwa
ni kushirikiana na wadadisi kwa kujibu maswali kwa usahihi na ufasaha
bila ya kuficha ukweli wa taarifa.
Awali akiongea wakati akimkaribisha Mgeni Rasmi kwa niaba ya Mtakwimu
mkuu wa Serikali Afisa Takwimu Muandamizi kutoka Ofisi ya Taifa ya
Takwimu Robert Kasililwa alisema kila mwananchi ashirikiane na
wadadisi kutoa taarifa sahihi ili serikali iweze kupanga mipango ya
maendeleo endelevu katika sekta ya kilimo itakayosaidia kuongeza wigo
wa kupunguza umaskini wa wananchi.
Alisema mafunzo hayo kitaifa yalianza siku ya Jumamosi wiki iliyopita
kwa jumla ya wadadisi 322 nchi nzima kupatia mafunzo ya matumizi ya
teknolojia mpya ya ukusanyaji wa Takwimu kwa mfumo wa Vishikwambi na
kuachana na mfumo uliopita wa matumizi ya karatasi unaogharimu fedha
nyingi.
Alisema kuwa teknolojia ya kisasa ambayo itapunguza gharama za
kukusanya na kuchakata takwimu kwa kiasi kikubwa sana tofauti na
sensa ya mwaka 2007/8 ambayo ilitumia takribani bilioni 10 huku sensa
hii ya mwaka 2019/20 ikitumia pungufu bilion 6 kwa pande zote za
Muungano Aidha matumizi hayo ya teknolojia hiyo itarahisisha
upatikanaji wa takwimu kwa muda mfupi na ubora zaidi tofauti na huko
nyuma.