Mwalimu ahukumiwa kifungo kwa kumpiga mwanafunzi wa darasa la saba

MPEKUZI |Page 1087, Chan:67282118 |RSSing.com"
Mahakama ya wilaya ya Makete imemhukumu mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Iwale Steven Mahenge kulipa faini ya sh. Laki 5 ama kwenda jela miezi minne kwa kosa la kumpiga na kumjeruhi mwanafunzi wake anayesoma darasa la 7 mwenye umri wa miaka 13 ambaye jina linahifadhiwa
Aidha mahakama hiyo imetoa amri kwa mshtakiwa kulipa fidia ya sh. Laki 1 kwa mlalamikaji kutokana na kosa alilomtendea lililopelekea kudhurika mwili wake
Hakimu Mkazi wa mfawidhi wa mahakama hiyo John Mpitanjia amesema shitaka hilo ni rufaa iliyokatwa na mlalamikaji kutoka mahakama ya Mwanzo ya Matamba baada ya kuona kwamba hakuridhika na hukumu iliyotolewa na mahakama hiyo ya mwanzo
Amesema katika shauri hilo baada ya mahakama kupitia mwenendo wa kesi iliyosikilizwa na mahakama ya Mwanzo Matamba, imebainika alishtakiwa chini ya kifungu ambacho hakikiwa sahihi na hiyo ni kwa mujibu wa kifungu cha 241 cha sheria ya kanuni ya adhabu 16 kama kilivyofanyiwa marejeo 2002, mshtakiwa akikutwa na hatia alitakiwa kupewa adhabu ya kifungo cha miaka 5 jela
Hakimu Mpitanjia amesema kwa mujibu wa kifungu cha 21B cha Sheria ya Mahakama ya Mahakimu, amebatilisha adhabu iliyotolewa na mahakama ya mwanzo Matamba kumhukumu Mwalimu huyo kulipa faini ya shilingi laki 1 ama kwenda jela miezi miwili pamoja na kumlipa mlalamikaji fidia ya shilingi 87,000
Akijitetea mbele ya Mahakama hiyo kabla ya hukumu kutolewa, Mshtakiwa huyo Mwl. Staven Mahenge amesema kwa kuwa ni kosa lake la kwanza anaomba mahakama hiyo imsamehe na kumuachia huru kwa kuwa anafamilia inayomtegemea, na wanafanya kazi kwenye mazingira magumu
Kufuatia maombi hayo hakimu akatoa hukumu hiyo kwa mshtakiwa na kusema rufaa iko wazi kwa upande wowote ambao haujaridhika na hukumu hiyo aliyoitoa na wanatakiwa kukata rufaa ndani ya siku 30 kuanzia leo
Mnamo Februari 18, 2020 majira ya saa tatu asubuhi katika shule ya msingi Iwale wilayani Makete mkoani Njombe mshtakiwa alimpiga kwa fimbo na mateke mwanafunzi wake (jina linahifadhiwa) na kupelekea kumjeruhi kwa kumvunja mkono wake