Prf kabudi apokea hati ya utambulisho

Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba
John Kabudi (Mb) amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Mratibu Mkazi
wa Shughuli za Umoja wa Mataifa (UN) Bw. Zlatan Milišić Pamoja na
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi
Duniani (UNHCR) Bw. Antonio Canhandula Jijini Dar es Salaam.


Waziri
Kabudi amewaeleza Bw. Milišić na Bw. Canhandula kuwa UN pamoja na UNHCR
zimekuwa na mchango mkubwa kwa kuiunga mkono Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania katika kukuza maendeleo pamoja na zile za
kushughulikia masuala ya wakimbizi.

“Kwa
ujumla UN imekuwa ikisaidia Tanzania kufanikisha agenda zake za
maendeleo endelevu ya kijamii, na kiuchumi hivyo Serikali itaendelea
kuhakikisha inaendeleza uhusiano huu,” Amesema Prof. Kabudi.

Kwa
upande wake Mratibu Mkazi wa Shughuli za Umoja wa Mataifa nchini (UN)
Bw. Milisic amesema kuwa uhusiano wa UN na Serikali ya Tanzania ni wa
muda mrefu na hivyo ni jukumu la UN kuhakikisha inaimarisha uhusiano huo
na kuuboresha.

 “Ni
matumaini yangu kuwa uhusiano huu tutauboresha vizuri na kuimarisha kwa
maslahi mapana na maendeleo endelevu ya taifa la Tanzania,” Amesema Bw.
Milišić

Nae
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi
Duniani (UNHCR) Bw. Canhandula amesema wanatambua mchango mkubwa ambao
Tanzania imekuwa ikiutoa kuhakikisha inaimarisha ulinzi wa maeneo ya
wakimbizi ili wananchi wa maeneo hayo waendelee kuishi kwa amani na
utulivu pamoja na kupatiwa mahitaji muhimu kama vile malazi na mavazi.

“Kwa
kweli UNHCR tunafurahishwa na jinsi Serikali ya Tanzania ambavyo
imekuwa ikipokea wakimbizi na kuwapatia baadhi ya mahitaji
muhimu……tunaomba tuendeleze ushirikiano huu kwa maendeleo yetu,” Amesema
Bw. Canhandula.