Nchi wanachama wa sadc kuimarisha sera na kujenga mikakati ya pamoja ya kukuza ajira kwa vijana

Na; Mwandishi Wetu

Nchi
Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zimejizatiti
kuimarisha Sera na kujenga mipango ya pamoja itakayowezesha kukuza
ajira kwa vijana katika Ukanda huo.

Akifungua
Mkutano wa Makatibu Wakuu, Maafisa Waandamizi na Wadau wa Utatu wa
Jumuiya hiyo wanaosimamia Sekta ya Kazi na Ajira hii leo Machi 2, 2020
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira
na Wenye Ulemavu Bw. Andrew Massawe alisema kuwa Mkutano huo
umewakutanisha Wataalamu wa sekta ya Kazi na Ajira kwa lengo la kuandaa
nyaraka mbalimbali zitakazo jadiliwa katika Mkutano wa Mawaziri ambao
utafunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Samia Suluhu Hassan tarehe 5 hadi 6 Machi, 2020 katika Kituo cha
Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere.

Alieleza
kuwa ajenda zitakazo jadiliwa ni pamoja na masuala ya kisera kuhusu
ukuzaji wa ajira kwa vijana, pia masuala yanayohusisha uhamaji wa nguvu
kazi ndani ya jumuiya ya SADC ambapo itasaidia pia kutoa fursa ya kukuza
ajira kwa nguvukazi ya nchi wanachama.

“Itambulike
kuwa uimarishwaji wa sera katika sekta ya kazi na ajira utasaidia kwa
kasi kikubwa kuwa chachu ya maendeleo ya nchi wanachama wa Jumuiya ya
maendeleo kusini mwa afrika endapo itasimamiwa vizuri,” Alisema Massawe

Aliongeza
kuwa kauli mbiu ya Mkutano huo isemayo “Kukuza Soko la Ajira na
Mahusiano Mema Sehemu za Kazi kwa Maendeleo Endelevu” inaelezea umuhimu
wa sekta ya kazi na ajira katika kuongeza tija ya ukuaji wa soko la
ajira kwa nchi wanachama.

Naye
Naibu Katibu Mtendaji mwenye dhamana ya Utangamano wa Kikanda, Dkt.
Thembinkosi Mhlongo alieleza kuwa mapendekezo yaliyotolewa katika
mkutano uliofanyika mwezi Novemba 20, 2019 ulioshirikisha wataalamu na
wadau wa utatu umechangia katika kujenga miongozo sahihi na sera
zitakazo wawezesha nchi wanachama wa SADC kukuza sekta ya kazi na ajira.

Kwa
Upande wake Mkurugenzi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Bw. Ally Msaki
alisema kuwa Mkutano wa Mawaziri utakao funguliwa rasmi tarehe 5 Machi,
2020 utawawezesha Mawaziri wa Nchi wanachama wa SADC kujadili kwa pamoja
ajenda mbalimbali zitakazokuwa zimepitiwa kwenye kikao cha wataalam kwa
lengo la kuimarisha sekta ya kazi na ajira nchini na jumuiya hiyo kwa
ujumla.

Hadi
sasa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)
zilizoshiriki katika Mkutano huo ni Angola, Afrika Kusini, Botswana,
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Msumbiji, Zambia, Zimbabwe, Malawi,
Namibia, Eswatini, Lesotho, Jamhuri ya Shelisheli na Tanzania.