Wakandarasi mradi wa maji tabora watakiwa kuongeza kasi ya utekelezaji

Na Mwandishi Wetu,Tabora
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga
amewataka wakandarasi wanaojenga mradi wa maji wa Tabora, Igunga, Nzega, Uyui
na Tabora kuongeza kasi ya utekelezaji wake ili ukamilike kwa wakati.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto)
akikagua na kutoa maelekezo ya utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa maji wa
Tabora, Igunga, Nzega na Uyui
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga
(katikati) akipokea maelezo ya ujenzi wa mradi kutoka kwa Mhandisi Mshauri wa
ujenzi wa mradi wa maji wa Tabora, Igunga, Nzega na Uyui wakati wa ziara yake
kwenye mradi huo.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto)
akitoa maelekezo kwa wakandarasi wanaotekeleza ujenzi wa mradi wa maji wa
Tabora, Igunga, Nzega na Uyui wakati wa ziara yake kwenye mradi huo.
Ujenzi ukiendelea kwenye moja ya eneo la mradi wa maji wa
Tabora, Igunga, Nzega na Uyui

Mhandisi Sanga ametoa maelekeo hayo Mkoani Tabora Februari 4,
2020 wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji
mkoani humo.
Mara baada ya kutembelea eneo la mradi huo na kujionea hatua
iliyofikiwa, Mhandisi Sanga alizungumza na wakandarasi wanaoutekeleza ambapo
alieleza kuridhishwa kwake na hatua iliyofikiwa. 
Hata hivyo, licha ya kuridhishwa na ubora wa ujenzi wa mradi,
Mhandisi Sanga aliwataka wakandarasi hao kuelekeza nguvu zaidi kwenye kazi
zinazopelekea wananchi kupata maji kwanza badala ya kuweka nguvu kubwa kwenye
maeneo mengine.
“Pamoja na kazi nzuri inayoonekana kufanyika maaelekezo yangu ni
kuwa wakandarasi wote mhakikishe kuwa kazi zinazofanyika kwa sasa ni zile
ambazo wananchi wataanza kupata maji mapema iwezekanvyo badala ya kuweka nguvu
kwenye majengo na mambo mengine,“ alisisitiza Mhandisi Sanga. 
Alibainisha kuwa wananchi wamesubiri mradi huo kwa muda mrefu na
kwamba kwakuwa tayari kumefanyika kazi kubwa wahakikishe maeneo machache ambayo
bado hayajakamilika wanayakamilisha. 
“Mnapaswa kuelewa wananchi wameusubiri mradi huu kwa muda mrefu,
hizi kazi zilizobakia mhakikishe zinakamilika haraka, shughuli zingine kama
kupaka rangi majengo zitafanyika baada ya kuwa tayari wananchi wanapata
huduma,” aliongeza Mhandisi Sanga. 
Kwa upande wao Wakandarasi hao walimhakikishia Naibu Katibu Mkuu
kutekeleza maelekezo aliyoyatoa na waliahidi kuhakikisha wanaongeza kasi ya
ujenzi wa mradi ikiwa ni pamoja na kufanya kazi hadi muda wa ziada ili tu inapofika
Februari mwishoni maji yawe yamefika kwenye maeneo yote yaliyokusudiwa ya
Tabora mjini, Nzega, Igunga na Uyui.
Mradi wa maji wa Tabora, Igunga, Nzega na Uyui unajengwa na
Kampuni tatu kutoka India ambazo ni Megha Engineering Infrastructures, L&T
na Afcons kwa gharama ya shilingi  Bilioni 602 zikiwa ni fedha za mkopo
kutoka benki ya Exim ya India. 
Mradi huo unatekelezwa kwa kipindi cha miezi 30 kutoka Agosti
2017 na unatakiwa kukamilika tarehe 23 Februari, 2020 kwa mujibu wa mkataba na
kwamba kukamilika kwake kutawezesha jumla ya wananchi 1,200,000 kunufaika na
huduma ya maji kutoka Ziwa Victoria.