Gst yaibua maeneo mapya utalii wa jiolojia…..kamati yataka sheria ya mri kuharakishwa

Taasisi
ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imewezesha kuibuliwa
maeneo Mapya ya Utalii wa Jiolojia kufuatia kukamilika kwa utafiti wa
Jiolojia katika maeneo ya ramani  Nne (4) za Jiolojia  (QDS 38,39,52 na
53).


Hayo
yameleezwa na Mtendaji Mkuu wa GST  Dkt. Mussa Budeba wakati
akiwasilisha taarifa  kuhusu Utekelezaji na Hali ya upatikanaji wa fedha
za maendeleo kwa taasisi hiyo kwa kipindi cha Nusu Mwaka  kwa Mwaka wa
Fedha 2019/20 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Dkt.
Budeba ameeleza kuwa, GST ilifanya utafiti huo kwa kushirikiana na
Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro na kuongeza kuwa, suala hilo limeongeza
vituo vya utalii wa Jiolojia nchini.

Akizungumzia
huduma za  maabara ya GST kwa wadau wa sekta ya madini, kilimo na
ujenzi amesema kuwa, baada ya kufanya maboresho  mbalimbali ikiwemo
ununuzi wa baadhi ya vifaa vya kisasa, kuboresha mifumo ya uendeshaji wa
maabara na kutoa mafunzo kwa watumishi, GST iliweza kupata ITHIBATIya
kimataifa ya uchunguzi wa sampuli za dhahabu kwa njia ya tanuru kutoka
shirika la SADCAS.

Aidha,
akizungumzia mafanikio ya taasisi hiyo ameyataja kuwa ni pamoja na
kushiriki katika mashindano ya kuchakata visawe vya mbali (Remote
Sensing) yaliyofanyika nchini Botswana na kushinda nafasi ya Nne ambapo
mwakilishi mmoja kutoka GST alitunukiwa Cheti cha kuwa mkufunzi kwa nchi
za Kusini mwa Afrika (SADC).

Dkt.
Budeba ameyataja mafanikio mengine ni kuweza kukusanya na kuhakiki
jumla ya taarifa 109 kutoka kwenye kampuni mbalimbali za utafiti na
uchimbaji wa madini pamoja na kukamilisha kazi ya ugani wa jiolojia na
jiokemia katika QDS 293 iliyopo katika maeneo ya wilaya ya Nachingwea na
Ruangwa mkoani Lindi.

Akizungumzia
tukio lililosadikiwa kuwa ni volcano lililotokea katika Kata ya
Ndembezi Manispaa ya Mji wa Shinyanga, ameieleza kamati kuwa, uchunguzi
uliofanywa na GST ulibaini kwamba kulikuwa na tope lililochanganyika na
maji likiwa linabubujika kutoka ardhini na kutengeneza rundo kubwa la
tope la udongo juu ya uso wa ardhi mfano wa kichuguu na kwamba tukio
hilo kwa lugha ya kigeni hujulikana kama ” liquefaction”.

‘’Mheshimiwa
Mwenyekiti matukio haya ni ya kawaida kutokea katika maeneo ambayo ni
tambarare, yenye kiasi kingi cha maji ardhini na pindi pakitokea msukumo
ama mgandamizo katika  matabaka ya miamba ardhini, husababisha
chembechembe za udongo kuchanganyika na maji na kusababisha tope ambalo
husukumwa kuja juu ya  uso wa ardhi ambapo tukio hilo hutokea,’’ amesema
Dkt. Budeba.

Naye,
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dustan
Kitandula akizungumza katika kikao hicho, ameitaka kuharakishwa suala la
kuandaliwa Sheria ya Chuo cha Madini kutokana na umuhimu wa chuo hicho
kuzalisha wataalam wa sekta ya madini na kutaka zifanyike jitihada
mahusus kukamilishwa suala hilo. Mwenyekiti Kitandula ametoa msisitizo
baada ya wajumbe wa kamati hiyo kutaka suala hilo kukamilishwa haraka.

Pia,
Mwenyekiti na wajumbe wa kamati hiyo wameishauri wizara kupitia chuo
hicho kuangalia namna ya kuzalisha wataalam zaidi na ambao watakuwa na
uwezo wa kujiajiri wenyewe bila kutegemea ajira ili kuwawezesha
watanzania wengi zaidi kushiriki katika shughuli za madini hususan
kwenye uchimbaji.

‘’ Najua hili si jambo la leo lakini ni vizuri kama wizara mkaanza kulitafakari,’’ amesema Mwenyekiti, Kitandula.

Awali,
akitoa taarifa kwa Kamati, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Madini Emmanuel
Kapira ameieleza kuwa, tayari Rasimu ya Sheria ya kuanzishwa kwa Chuo
cha Madini imeandaliwa na kupelekwa katika Mamlaka husika kwa hatua
zaidi.

Pia,
Kapira ameieleza kamati hiyo kuwa, katika kuwasaidia wachimbaji wadogo
kupata mafunzo yanayotolewa chuoni hapo, kimetengeneza mfumo wa
kufundisha kwa lugha ya Kiswahili kwa waajiriwa na wachimbaji.

Naye,
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo amesema ipo haja ya wadau wa
madini kujifunza elimu ya biashara ya madini  kwa kuzingatia fursa
zilizopo katika sekta hiyo na kuongeza kuwa, suala  hilo linatoa nafasi
nzuri  ya kibiashara na uwekezaji kupitia sekta ya madini . Aidha, Naibu
Waziri Nyongo ameishukuru kamati hiyo kwa kuendelea kuishauri wizara
ili iweze kusimamia vema sekta ya madini.

Kwa
upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila
akitolea ufafanuzi suala la maabara ya GST baada ya kupata ITHIBATI ya
Kimataifa, amewaomba wajumbe wa kamati hiyo kusaidia kutoa elimu kwa
wadau  wa madini katika maeneo yao ili waweze kutumia maabara hiyo
ikizingatiwa kuwa  gharama zake ni nafuu na ina viwango vya kimataifa.

Akizungumzia
suala la Chuo cha Madini kulelewa na Chuo Kikuu cha Dar es salaam,
amesema pamoja na mambo mengine ni kukiwezesha kuwa bora zaidi na
kuendesha programu zinazoendana na soko la ajira.

 Vikao
kati ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini na Wizara ya Madini
vilivyoanza Januari 20, vimehitimishwa leo Januari 22, 2020.

Chanzo: Wizara ya Madini