Mv- mwanza kustawisha biashara kanda ya ziwa, na nchi jirani za kenya na uganda

Na.Paschal Dotto-MAELEZO.

Serikali
inaendelea na utekelezaji wa miradi mingi ya kuimarisha miundombinu
katika sekta mbalimbali ikiwemo mradi ya umeme (JN HPP-Julius Nyerere
Hydropower project) kwa gharama ya shilingi trilioni 6.5, Ujenzi wa Reli
ya Kisasa SGR kwa gharama ya shilingi trilioni 7 na miradi mingine
ambayo itaweka mazingira wezeshi kwa wananchi kufanya biashara na
uwekezaji.


Mnamo
Desemba 8, 2019, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John
Magufuli alizindua ujenzi wa mradi mwingine mkubwa wa ujenzi wa meli
kubwa ya abiria na mizigo ya MV. Mwanza, ukarabati wa meli za MV.
Victoria na MV. Butiama pamoja na ujenzi wa chelezo katika lango la
biashara na uchumi kanda za ziwa ambao utekelezaji wake unaendelea
vizuri na utakapokamilika utakuwa umegharimu zaidi ya shilingi bilioni
153.7.

Meneja
wa mradi huo, Mhandisi Abel Gwanafyo ameeleza kuwa, meli kubwa ya “MV
Mwanza, Hapa Kazi Tu” itakayogharimu shilingi bilioni 89.76 ambayo
ujenzi wake unatekelezwa na kampuni ya ujenzi ya GAS ENTEC
wakishirikiana na KANG NAM kutoka Korea Kusini pamoja na SUMA JKT kutoka
Tanzania, itakuja kuwa mbadala ya Meli ya MV Bukoba ambayo ilizama
miaka 23 ilipita.

 Katika
kampeni za uchaguzi mkuu wa 2015, Rais wa Awamu ya Tano, Dkt John Pombe
Magufuli aliwaahidi wananchi wa kanda ya ziwa kuwa atajenga meli kubwa
kuwaenzi waliokufa kwenye ajali hiyo lakini pia kuimarisha usafirishaji
katika ukanda huo wa Tanzania kwani kuna fursa nyingi za biashara.

“Ni
miaka 23, tangu kuzama meli ya MV. Bukoba mwaka 1996, miaka mingi
imepita, lakini pia kuharibika kwa meli ya mizigo kumekuwa na tatizo
kubwa kwa sekta ya usafarishaji kwa wananchi wanaioshi kuzunguka ziwa
Victoria na hivyo kuathiri shughuli za uchumi na uzalishaji Kanda ya
Ziwa”, Rais Dkt. John Magufuli.

Mradi
huo mkubwa utakwenda sambamba na miradi mingine ya ukarabati wa meli ya
Mv Victoria utaogharimu shilingi bilioni 22.71, Mv Butiama bilioni 4.9,
ambazo ujenzi wake unatekelezwa na kampuni ya ujenzi ya KTMI kutoka
Korea Kusini huku ujenzi wa chelezo utakaogharimu shilingi bilioni 36.4,
unatekelezwa na kampuni ya Stx Engine ikishirikiana na SAE Kyong kutoka
Korea Kusini.

MV
Mwanza Hapa Kazi Tu, itakuwa na urefu wa mita 92, na uwezo wa kubeba
abiria 1,200, mizigo tani 400, magari makubwa 3 na magari madogo 20,
huku Mv Victoria ikibeba abiria 1,200, mizigo tani 200 na Mv Butiama
abiria 200, tani 100, na kuwezesha zaidi ya abiria 2,600 na tani 700 za
mizigo kwa wakati mmoja hivyo kusadia kupunguza adha ya usafiri na
usafirishaji kwa abiria na mizigo katika ukanda huo wa ziwa.

“Ni
wazi kuwa utekelezaji wa miradi hii utakaogharimu shilingi bilioni
153.7 utasaidia sana kutatua tatizo la usafiri na usafirishaji kwa
wananchi wanaoishi kando ya ziwa Victoria, siyo tu hapa nchini bali hata
kwa jirani zetu Kenya na Uganda kwa hiyo ni miradi ambayo ina manufaa
kwa uchumi wetu”, amesema Rais Magufuli.

Aidha
kukamilika kwa mradi huu kutaondoa kwa kiasi kikubwa tatizo la usafiri
kwa abiria katika ukanda huo wa ziwa ikiwa ni pamoja na usafirishaji wa
mizigo na mazao mbalimbali ya biashara na kuzalisha ajira kwani meli hii
itahitaji wafanyakazi wa aina mbalimbali. Kwa upande wa nchi jirani za
Kenya na Uganda , hii pia itakuwa fursa kwao kusafirisha mazao ya
biashara na chakula kupitia ziwa Victoria badala ya kutegemea usafiri wa
aina moja wa barabara au wa anga.

 Katika
uzinduzi wa ujenzi wa mradi huo ambao utafungua ukanda wa kibiashara na
kusaidia kukuza pato la taifa, Rais Magufuli alieleza dhamira kubwa ya
Serikali ya Awamu ya Tano kuwa ni kufanya mabadiliko makubwa kwa kuleta
miradi wezeshi kwa wananchi bila kutegemea misaada yenye masharti lukuki
na ufadhili.

Sekta
hii ya usafirishaji kwa njia ya maji ni muhimu sana na Serikali kupitia
Mamlaka ya Bandari Tanzani (TPA), pamoja na Shirika la Huduma za Meli
imekuwa na usimamizi madhubuti ili kukuza  na kuimarisha sekta hiyo
ambayo ni nyenzo kubwa katika uchumi.
Kampuni
ya Huduma za meli iliyoanzishwa na Baba wa Taifa, Mwl. Julius Nyerere
kwa sasa inafanya kazi kubwa baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani
na kuelekeza nguvu katika kuimarisha bandari nchini. Hapo awali ziwa
Victoria lilikuwa meli 14 ikiwemo meli ya utalii, lakini meli hiyo
iliacha kufanya kazi kutokana na uongozi mbovu, ikiwa ni pamoja na
vitendo vya wizi na ubadhilifu wa mali za umma  na hatimaye meli zote 14
ziliisha na kubaki moja tu.

“Nawapongeza
Kampuni ya Huduma za Meli kwa kuboresha utendaji kazi katika kampuni
hii, kwani miaka ya nyuma hata mishahara mlikuwa hamuwezi kulipa
wafanyakazi wenu, lakini kwa sasa utendaji kazi uko vizuri na umeimarika
ambapo mpaka sasa meli nne zipo na zinafanya kazi. Meli hizo ni Mv
Clarius, Mv Umoja, Mv Sangara na Mv Wimbi, kwa hiyo ujenzi wa meli mpya
na ukarabati wa meli hizi mbili utasaidia kukuza huduma zenu”,
alisema,Rais Magufuli.

Mamlaka
ya Bandari imekuwa ikiendelea na upanuzi na ujenzi wa bandari
mbalimbali nchini zikiwemo bandari ya Dar es Salaam, Mtwara, Tanga,
Mwanza na bandari zake ndogondogo za Kemendo, Bukoba, Kwemukwikwi na
Nyamirembe kwa upande wa kanda ya ziwa.

 Mhandisi,Gwanafyo
ameeleza kuwa ujenzi wa meli mpya “Mv Mwanza Hapa Kazi Tu” umefikia
asilimia 52 tofauti na mwezi Desemba 2019 ambapo ulikuwa asilimi 50,
huku ukarabati wa Mv Victoria ukiwa asilimia 75 badala ya 65, Mv Butiama
asilimi 70 badala ya 60 huku ujenzi wa chelezo ukiwa ni asilimia 80
badala 68 za mwezi Desemba 2019.

Miradi
hiyo imeweza kutoa fursa nyingi kwa wananchi wa mkoa wa Mwanza ikiwemo
fursa za biashara na ajira kwani mpaka sasa kuna ajira zaidi ya 1,000 na
bado zinaongezeka kwa kadri siku zinavyoongezeka.

Ujenzi
wa meli hii kubwa ni utekelezaji wa ahadi na kutimiza maono ya Baba wa
Taifa Mwl.Julius Nyerere aliyetaka kuwepo na meli kubwa katika ukanda
huo wa kiuchumi wa Tanzania, ambapo mwaka 1979, alisimamia kuundwa kwa 
meli ya MV Bukoba ambayo  ilizama mwaka 1996 na kuleta ugumu wa usafiri
na usafirishaji katika ziwa Victoria ambalo ni tegemeo kwa wananchi wa
kanda hiyo pamoja na nchi jirani. Uamuzi wa  Rais Magufuli wa kujenga
meli hiyo kubwa ‘Mv Mwanza, Hapa Kazi Tu’ na kukarabati meli nyingine
unaonyesha jinsi alivyodhamiria kuyaishi na kuyatekeleza maono ya Baba
wa Taifa, Mwalimu Nyerere kwa vitendo.

Mwisho