Mwanamke anaswa amebeba vipodozi haramu akidai ni mtoto

Mwanamke akiwa amebeba vipodozi bandia vyenye muonekano wa mtoto mdogo.
Maafisa wa polisi nchini Uganda, wamemkamata mwanamke mmoja aliyekuwa
akivuka mpaka wa nchi hiyo kutokea nchini Congo, akiwa amebeba vipodozi
haramu alivyokuwa amevifungasha na kuvivalisha kwenye nguo ya mtoto,
ambayo ilileta uhalisia wa mtoto mdogo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamishna wa Bidhaa nchini Uganda,
Dickson Kateshumbwa, amesema kuwa bidhaa hizo zilikuwa zimepakiwa vyema
katika nguo za mtoto ili kuonekana kwamba ni mtoto, huku Mamlaka ya
Mapato nchini Uganda (URA), ikisema kuwa tayari imekwishaitambua mbinu
hiyo, hivyo si rahisi kwa msafirishaji yeyote wa vipodozi bandia kupita
salama nchini humo. 
“Mtoto ghushi alipandishwa gari la kutoka Congo katika kituo cha mpaka
wa Mpondwe, na baadae iligundulika mtoto huyo kuwa ni mwanasesere
aliyekuwa amesakamiwa vipodozi haramu, baadhi ya walanguzi huendelea
kushangaza” alisema Kateshumbwa. 
Serikali ya Uganda ilipiga marufuku vipodozi hivyo tangu mwaka 2016, kwa
sababu ya kuwa na viwango vya madini ya zebaki na hydroquinone, ambapo
utafiti kadhaa umefichua kuwa vina madhara kwa afya, ambapo pia Idara ya
Ubora wa Bidhaa (KEBS), iliorodhesha baadhi ya mafuta na bidhaa za
urembo ambazo zilikosa, kutimiza masharti ya ubora mnamo Novemba 2019.