Maafisa tarafa nchini watakiwa kushiriki vikao vya kamati za kudumu na baraza la madiwani ili kusimamia vyema shughuli za maendeleo

Na Happiness Shayo, Iramba-Singida

Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) amewataka Maafisa Tarafa nchini kushiriki
vikao vya Kamati za Kudumu na Baraza la Madiwani ili kurahisisha
utendaji kazi hasa katika usimamizi wa  shughuli za maendeleo katika
maeneo yao ya kazi.

Agizo
hilo amelitoa wakati wa kikao kazi na watumishi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Iramba chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji, kabla ya
kutembelea  wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika
halmashauri hiyo.

“Kwa
mujibu wa Mwongozo wa Uwajibikaji wa Makatibu Tarafa katika Wilaya na
Halmashauri za Serikali za Mitaa wa mwaka 2003 ni haki ya msingi kwa
Afisa Tarafa kuhudhuria vikao vya Kamati za Kudumu na Baraza la Madiwani
vya Halmashauri ili kutoa ushauri  pamoja na taarifa za utekelezaji wa
shughuli zilizofanyika katika eneo lake” Dkt. Mwanjelwa amefafanua.

Dkt.
Mwanjelwa amesema kuwa Maafisa Tarafa wasipopewa nafasi za kushiriki
katika vikao vya Kamati za Kudumu na Baraza la Madiwani, hoja za msingi
za kimaendeleo hazitawasilishwa hivyo maendeleo yatakwamishwa katika
halmashauri wanazozihudumia.

Dkt.
Mwanjelwa ameweka bayana kuwa ni muhimu Maafisa Tarafa, Makatibu Tawala
na Wakurugenzi wa Halmashauri wakafanya kazi kwa kushirikiana ili
kuongeza ufanisi katika shughuli za maendeleo.

Aidha,
Mhe. Dkt. Mwanjelwa amewataka Watendaji wa Halmashauri kujenga
utaratibu wa kufanya vikao na watumishi ili kusikiliza kero zao na
kuzitatua.

“Hakikisheni
mnatenga muda wa kuongea na Watumishi walio chini yenu ili kuwaelimisha
kuhusu nyaraka mbalimbali za kiutumishi pamoja na kusikiliza kero na
maoni yao na kuyafanyia kazi” Dkt. Mwanjelwa amesisitiza.

Mhe.Dkt. Mwanjelwa yupo katika ziara ya kikazi Mkoani Singida kwa lengo la kukagua utekelezaji wa shughuli za TASAF