Elimu juu ya sekta ya madini inatakiwa morogoro

Na Tito Mselem Dodoma,

Waziri
Biteko ameagiza uongozi wa Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana na Wizara
ya Madini kuandaa maonesho ya madini kwa lengo la kuelimisha Umma kwa
watu wa Morogoro na mikoa jirani juu ya Sheria, Kanuni na fursa zilizopo
katika Sekta ya Madini.

Hayo
yamebainishwa leo January 08, 2020 na Waziri wa Madini Doto Biteko,
alipofanya kikao na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Sanare,
kilichofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Madini, Mtumba jijini Dodoma.

“Nichukue
fursa hii kuwaelekeza wataalamu wote wa Wizara ya Madini na Taasisi
zake kuhakikisha wanashirikiana na Mkoa wa Morogoro kuzitangaza fursa
zinazopatikana katika Sekta ya Madini Mkoani Morogoro kwa kutumia njia
mbalimbali ikiwemo kuandaa maonesho yatakayopelekea kuelimika kwa
wananchi wa Mkoa huo,” alisema Waziri Biteko. 

Aidha,
Waziri Biteko amesisitiza ushirikiano katika kusimamia Sekta ya Madini
kati ya Wizara na Mkoa wa Morogoro na kumpongeza Afisa Madini Mkazi wa
Mkoa wa Morogoro Emmanuel Shija kwa kazi nzuri anazozifanya katika
ukusanyaji wa mapato ya serikali.

Waziri
Biteko amesema maendeleo ya Sekta ya Madini katika Mkoa wa Morogoro
yatatokana na wachimbaji wenyewe, hivyo Wizara na Mkoa inapaswa
kuwalinda na kuwalea wachimbaji na wadau wote wa madini mkoani humo.

Akizungumzia
changamoto inayowakabili wananchi wa Morogoro Biteko alisema ni pamoja
na uelewa mdogo walionao juu ya masuala yanayohusiana na Sekta ya Madini
kuwa ni kikwazo katika kupelekea maendeleo Mkoani humo.




Kwa
upande wake, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, ameonesha
kufurahishwa na kitendo cha Mkoa wa Morogoro kuonesha mafanikio makubwa
katika makusanyo ya mapato ya serikali kutoka shilingi 811,714,294.12
kwa mwaka 2017/2018 mpaka kufikia 1,031,865,068.41 kwa mwaka 2018/2019.

“Madini
ya Ujenzi, Vito na Dhahabu tukiyasimamia vizuri hakika yatatuingizia
fedha nyingi watu wa Morogoro, hivyo nikuombe Mkuu wa Mkoa ukalifanyie
kazi hilo, pia sisi kama Wizara ya Madini tutashirikana na Mkoa wa
Morogoro kuhakikisha wawekezaji wanakuja kuwekeza katika Sekta ya Madini
Mkoani Morogoro,” alisema Nyongo.

Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Sanare, amemuomba Waziri
kupatiwa ushirikiano katika kuitangaza Morogoro kuwa ni Mkoa wa Madini
na sio kilimo peke yake.

Pia
Sanare, amesema, Mkoa wa Morogoro unampango wa kufufua viwanda vya
Ceramics vilivyokuwepo ili kuongeza matumizi ya madini ya  viwandani
yanayopatikana katika Mkoa huo kwa wingi na kuendeleza uhamasishaji wa
uanzishwaji wa viwanda vipya vya Ceramics.

Wakati
huo huo, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Morogoro, Emmanuel Shija,
amesema Mkoa wa Morogoro una Jumla ya leseni 3082 za wachimbaji wadogo
kati yake ni leseni 250 tu ndizo zinafanya kazi ya uzalishaji, hivyo
Ofisi ya Madini inaendelea na zoezi la kufuta leseni zote zenye makosa.

“Mwaka
2019 jumla ya leseni 223 zilifutwa na jumla ya hati za makosa kwa
leseni 836 zimetolewa, leseni hizo ziko kwenye utaratibu wa kufutwa
ndani ya mwaka huu wa fedha endapo wamiliki wa leseni hizo
hawatarekebisha makosa yao kama Sheria inavyoelekeza,” alisema Shija.

Kikao
hicho kilicholenga kujadili changamoto na maendeleo ya Sekta ya Madini
kwa Mkoa wa Morogoro ikiwa ni pamoja na kuangalia fursa zilizopo katika
Sekta ya Madini katika kuharakisha maendeleo ya mkoa huo, kilihudhuriwa
na viongozi mbalimbali wa Wizara ya Madini na Taasisi zilizo chini ya
Wizara akiwepo Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, Mtendaji Mkuu
wa Tume ya Madini Prof. Shukrani Manya, Mkurugenzi Taasisi ya Jiolojia
na Utafiti Tanzania Dkta Musa Budeba, Kamishna wa Madini Mhandisi David
Mulabwa, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya Madini Edwin
Egenge, Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Madini Augustine
Ollal na wengine.