Bomu lililotegwa ndani ya gari lawaua watu zaidi ya 40 mogadishu, somalia

Zaidi ya watu 40 wamedaiwa kuangamia kwenye mlipuko wa bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari Mogadishu nchini Somalia.


Bomu
hilo imeripotiwa lilipuka wakati wa pilka pilka nyingi asubuhi katika
kituo kimoja cha kukagua magari eneo la makutano ya barabara jijini
Mogadishu.

 
Walioshuhudia mlipuko wa bomu hilo wanasema kwamba idadi ya waliofariki dunia huenda ikaongezeka.

Kulingana na ripoti ya Shirika la Habari la BBC, walioshuhudia wamedai mlipuko huo ulikuwa mbaya zaidi.

Kufikia
sasa hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulizi hilo lakini kwa
kipindi kirefu wapiganaji wa kundi la al-Shabab wamekuwa wakitekeleza
mashambulizi ya mara kwa mara katika taifa hilo.

Tangu mwaka 2007 kundi la kigaidi la Al-Shabab limekuwa likifanya juu chini kuipindua serikali kuu ya Somalia.

Mwaka 2011, Al Shabab lilifurushwa kutoka mji mkuu Mogadishu kwa
ushirikiano wa jeshi la Somalia na vikosi vya Umoja wa Afrika
vilivyotumwa nchini humo AMISOM; hata hivyo hadi sasa kundi hilo la
kigaidi lingali linashikilia baadhi ya  maeneo ya vijijini nchini humo

Somalia ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1992 na
katika miaka ya hivi karibuni nchi hiyo imeshuhudia kushadidi hujuma za
magaidi wa kundi la al-Shabab na hivyo kuwasababishia raia wa nchi hiyo
matatizo makubwa.