Gari lagonga watu 12 mwanza

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Murilo
Mwanaume mmoja amefariki dunia na wengine kumi na moja kujeruhiwa baada
ya kugongwa na gari lililoacha njia na kuwagonga wakiwa pembezoni mwa
barabara ya Furahisha eneo la Mkunguni Jijini Mwanza. 
Tukio hilo limetokea majira ya saa 10:30 Alfajiri ambapo gari lenye
namba za usajili T 946 DPL TOYOTA Crawn kuacha njia na kuwagonga
wafanyabiashara ndogondogo pamoja na watembea kwa miguu waliokuwa
wakitoka kanisani kwenye mkesha wa Krismasi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Murilo amethibitisha kutokea
kwa tukio hilo na tayari dereva wa gari, Desisi Omary (29) anashikiliwa
na Jeshi la Polisi huku akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya
Rufaa ya Mkoani humo.
“Tukio hilo limetokea barabara ya Furahisha, lililopo eneo la Mkunguni
ambapo gari hilo liliwagonga wafanyabiashara ndogondogo pamoja na
watembea kwa miguu waliokuwa wakitoka kanisani na kusababisha kifo cha
mtu mmoja ambaye mpaka sasa bado hatujajua utambulisho wake”, amesema
Kamanda Murilo.
Kwa upande wake Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Sekou
Toure amesema wamepokea jumla ya watu 11, mmoja kati yao akiwa
ameshafariki na wengine 10 wakiwa majeruhi huku watano wakihamishiwa
Hospitali ya Rufaa ya Bungando.