Aliyekuwa mwanasheria iptl aunganishwa kesi ya kina sethi

Aliyekuwa mwanasheria wa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Joseph Makandege, ameunganishwa katika kesi na Mfanyabiashara Harbinder Sethi na Rugemarila  akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi ikiwamo kutakatisha Dola za Marekani 980,000.

 

Makandege amefanya idadi ya washtakiwa katika kesi hiyo kufika watatu na idadi ya mashtaka kufika 15 kutoka 12 ya awali.

Kigogo huyo ambaye pia alikuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, alisomewa mashtaka matano ya kula njama, kuratibu genge la uhalifu, kujipatia na kutakatisha fedha, mbele ya Hakimu Mkazi Thomas Simba wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

Jopo la Upande wa Jamhuri likiongozwa Mawakili wa Serikali Wakuu, Paul Kadushi, Faraja Nchimbi na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon.

Kadushi alidai kuwa katika tarehe tofauti kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi, 2014, mahali tofauti jijini Dar es Salaam, Sethi, Makandege na James Lugemarila walikula njama ya kutenda kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa siku ya tukio la kwanza, washtakiwa wote watatu, waliratibu genge la uhalifu kwa lengo la kujinufaisha wao wenyewe binafsi.

Nchimbi alidai Makandege anakabiliwa na shtaka la 13, kwamba kati ya Januari 23 na Februari 10, 2014, katika Benki ya Stanbic tawi la Centre lililoko Kinondoni na Benki ya UBL (T) Ltd iliyoko Ilala, mshtakiwa alijipatia kwa njia ya udanganyifu, Dola za Marekani 380,000 na 600,000.

Katika shtaka la 14, Upande wa Jamhuri ulidai kuwa katika benki za Stanbic na UBL, Makandege aliisabishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano hasara ya Dola za Marekani 980,000.

Wankyo alidai katika shtaka la 15, siku na tarehe ya tukio la 13, Makandege alitakatisha Dola za Marekani 980,000 wakati akijua ni zao la genge la uhalifu.

Mshtakiwa huyo hakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za ujumumu uchumi.

Upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na uliomba tarehe nyingine ya kutajwa na kumuunganisha mshtakiwa na wenzake.

Hakimu Simba alisema kesi hiyo itatajwa Januari 2, mwakani, mshtakiwa apelekwe mahabusu.