Serikali yabainisha fursa ya ufugaji samaki, kaa, kambakochi na majongoo bahari ukanda wa pwani.

Na. Edward Kondela
Serikali imesema inahakikisha sera yake ya kuhamasisha wananchi kufuga
samaki inatekelezwa kote nchini ili kutosheleza mahitaji ya soko la
samaki nchini pamoja na kukuza pato la taifa na mtu mmoja mmoja.

Akizungumza Mjini Mtwara, wakati akifungua tawi la Wakala ya Elimu na
Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Kampasi ya Mikindani Mkoani Mtwara, Naibu Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ameiagiza FETA kwa kushirikiana
na Idara ya Ukuzaji Viumbe kwenye Maji kutoka katika wizara hiyo,
kuandaa mitaala ya ufugaji viumbe kwenye maji wakiwemo samaki, kaa,
majongoo bahari na Kambakochi kwa ajili ya wananchi wa Ukanda wa Pwani
ili waweze kuongeza vipato vyao kupitia fursa ya ufugaji. PAUSE

Mhe. Abdallah Ulega – Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi

Aidha Mhe. Ulega ameagiza uundwaji wa vikundi vya uzalishaji kaa,
Kambakochi, majongoo bahari pamoja na wazalishaji wa zao la mwani ili
iwe rahisi kwa vikundi hivyo kutambulika rasmi pindi mazao yao
yanapohitajika sokoni, na watu waweze kufika katika mashamba yao ya
ufugaji kwa ajili ya kuvua samaki na viumbe vingine wakiwemo kaa,
kambakochi na majongoo bahari ambao wamekuwa na soko kubwa sana na
mahitaji yake kuongezeka katika baadhi ya maeneo zikiwemo hoteli za
kitalii.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mafunzo kutoka FETA Bw. Ambakisye Simtoe
amesema chuo hicho kimepanga kuzalisha wagani kwa ajili ya kuendeleza na
kukuza tasnia ya uvuvi nchini pamoja na kununua mashine ya kuzalisha
vifaranga bora ili iwe rahisi kwa wananchi wa Ukanda wa Pwani kupata
vifaranga hivyo kwa bei nafuu huku katika risala ya wanafunzi hao
wakisema mafunzo waliyoyapata yakiwemo ya ufugaji wa samaki
yatawawezesha kujiajiri. VOX

Bw. Ambakisye Simtoe – Mkurugenzi wa Mafunzo FETA

Bi. Monica Mfaume – Msoma risala kwa niaba ya wanafunzi

Jumla ya wanafunzi 62 wamehitimu kozi fupi ya ufugaji samaki katika chuo
cha FETA Kampasi ya Mikindani Mkoani Mtwara na kukabidhiwa vyeti na
mgeni rasmi Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ambaye
amekifungua rasmi chuo hicho chenye uwezo wa kudahili wanafunzi 240 kwa
mwaka.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi mahitaji ya soko
la samaki nchini ni Tani 700,000 hadi 800,000 kwa mwaka huku uzalishaji
ukiwa wastani wa Tani 400,000 hadi 450,000 hali ambayo Naibu Waziri
Ulega amesisitiza kwa chuo cha FETA Kampasi ya Mikindani Mkoani Mtwara
kuwa kampasi ya mfano katika kutoa mafunzo ya ufugaji samaki, kaa,
kambakochi na majongoo bahari ili wananchi waweze kutosheleza soko la
ndani na kukuza vipato vyao na taifa kwa ujumla.