Sheria ya fidia ya uharibifu wa wanyamapori kupitiwa upya


Serikali ya Tanzania ipo katika
hatua ya kupitia upya sheria ya fidia ya uharibifu unaofanywa na
wanyamapori  ili kuendana na wakati na gharama halisi  ya mazao
yanayoharibiwa na wanyama hao ili  kupunguza malalamiko ya wananchi juu
ya kutokupewa  fidia stahiki inayoendana na uharibifu hao.


Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa
Wizara ya Maliasili na Utalii ,Profesa Adolf  Mkenda wakati akizungumza
katika mkutano wa wadau wa uhifadhi na maliasili uliondaliwa na Jumuiko
la Maliasili nchini Tanzania (TRN) ,ambapo amesema kuwa sheria hiyo ya
mwaka 1974  inafanyiwa mapitio na kufanyiwa marekebisho ili wananchi
waweze kupata haki pale uharibifu unapotokea.


Profesa Mkenda asema kuwa
marekebisho yatakayofanyika yataweza kupunguza malalamiko yaliyokua
yakitolewa na wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi lakini pia wizara
hiyo imekua ikigawa mizinga ya nyuki kama njia mojawapo ya kukabiliana
na uharibifu wa wanyamapori hususan tembo.


Aidha amesema kuwa katika
kukabiliana na uwindaji wa kitoweo baada ya kufanikiwa kutokomeza
uwindaji haramu wa tembo kwa sasa wizara inakamilisha mchakato wa kuwa
na sehemu za kuuza nyama pori katika maeneo yanayozunguka hifadhi ili
kuepuka uwindaji wa kitoweo katika maeneo ya uhifadhi.


Mbunge wa Babati Vijijini Jitu
Soni  amesema kuwa kurekebishwa kwa sheria ya fidia kutawafuta wananchi
machozi hasa wanaoishi mbali kidogo na hifadhi tofauti na wale walioko
karibu na pia itasaidia kuhamasisha uhifadhi endelevu miongoni mwa
wananchi.


Mkurugenzi wa Jumuiko la Maliasili
nchini Tanzania Zacharia Faustine  amesema kuwa mchakato wa kulipa
fidia umekua ukichukua muda mrefu na kiasi wanacholipwa hakiendani na
hasara jambo ambalo linaweza kushusha hamasa wa wananchi kushiriki
katika uhifadhi hivyo serikali imefanya vyema kupitia sheria hiyo.


Mmoja wa wananchi wanaoishi
pembezoni mwa Hifadhi za taifa,Asha Salim  amesema kuwa marekebisho
sheria ya fidia imekua sio rafiki kwa wananchi hivyo inapaswa kuangaliwa
upya kwa maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla.