Picha : rc telack awaonya wafungwa waliopewa msamaha na rais magufuli


Mkuu
wa mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack, amewaonya wafungwa ambao
wamepewa msamaha wa kuachiwa huru na Rais John Magufuli kuwa
wakajishughulishe kwenye shughuli halali za kuwaingizia kipato, kikiwamo
kilimo, mifugo, pamoja na kufanya biashara mbalimbali na siyo kwenda
kufanya uhalifu tena.


Telack
ametoa onyo hilo leo, Desemba 10,2019 , wakati alipo kwenda Magereza
kujiridhisha majina ya wafungwa 74 mkoani Shinyanga kama ni kweli wale
ambao wamepewa msamaha na Rais Magufuli jana Jijini Mwanza, kwenye
maadhimisho ya miaka 58 ya uhuru na miaka 57 ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, kati ya wafungwa 5,533 waliosamehewa nchi nzima.


Amesema
kutokana na kipindi hiki ni cha msimu wa mvua, wafungwa hao 74 ambao
wameachiwa kwa msamaha wa Rais Magufuli mkoani Shinyanga, wanatakiwa
wakajikite kwenye shughuli za kilimo, mifugo, na kufanya biashara za
kuwaingizia kipato halali, na siyo kurudi kwenye uhalifu.


“Natoa
tahadhari kwenu nyie wafungwa ambao mmeachiwa huru kwa msamaha wa Rais
John Magufuli, msirudi uraiani kwenda kufanya matukio ya uhalifu tena,
na bahati nzuri mmeachiwa kwenye kipindi kizuri cha msimu wa mvua, hivyo
muende mkajishughulishe na kilimo ili mpate mavuno na kuinuka
kiuchumi,”
amesema Telack.


Naye
Mkuu wa Magereza mkoani Shinyanga Kamishina msaidizi wa Magereza Dk.t
Wilison Rugamba, amesema wafungwa ambao wameachiwa huru mkoani humo ni
wale ambao waliobakiza vifungo vyao kuanzia siku moja, miezi sita, hadi
mwaka mmoja, ambapo mkoani humo wameachiwa wafungwa 74, wa kiume 62 na
wanawake 12.


Nao
baadhi ya wafungwa hao akiwemo Bakari Juma mkazi wa Shinyanga,
wamemshukuru Rais John Magufuli kwa kutoa msamaha huo, huku wamkimuahidi
mkuu huyo wa mkoa kutokwenda kufanya uhalifu tena, ikiwa baadhi yao
wameshajifunza jinsi ya kilimo bora wakiwa magereza na wataenda
kuendelea ujuzi huo.


TAZAMA PICHA HAPA CHINI


Mkuu
wa mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack, akizungumza na wafungwa
walioachiwa huru kwa msamaha wa Rais John Magufuli kwenye Gereza la
Shinyanga na kuwaonya wasirudie kufanya uhalifu bali wakajikite kufanya
shughuli halali za kuwaingizia kipato. Picha na Marco Maduhu – Malunde 1 blog

Mkuu
wa Magereza mkoani Shinyanga Kamishina msaidizi wa Magereza Dkt Wilison
Rugamba, akitoa taarifa kwa mkuu wa mkoa, kuwa wafungwa 74 wameachiwa
huru mkoani Shinyanga, wanaume 62, wanawake 12.


Mfungwa
aliyeachiwa huru kwenye Gereza la Shinyanga Revocatus Medard, kwa
msamaha wa Rais John Magufuli, akishukuru kwa msamaha huo na kuahidi
kutofanya uhalifu tena.


Mfungwa
aliyeachiwa huru mkoani Shinyanga Bakari Juma kwa msamaha wa Rais John
Magufuli, akishukuru kwa msamaha huo na kuahidi kutofanya uharifu tena,
ambapo kwa sasa imebidi aokoke kabisa wakati akiwa humo Gerezani, na
kuahidi kwenda kufanya shughuli za kilimo, ikiwa ujuzi wa kulima
kitaalamu ameupata Gerezani.