Mbunge
wa Ndanda, Cecil Mwambe(Chadema), ametangaza azma ya kutaka kuwania
nafasi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
Taifa ambayo kwa sasa inashikiliwa na, Freeman Mbowe, anayemaliza muda
wake.
Mwambe ametangaza azma yake hiyo leo Jumanne Novemba 26, jijini Dar es
Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema
anaamini kuwa yeye ni mtu sahihi kuongoza jahazi hilo, tofauti na watu
wasio na nia njema na chama hicho wanavyosema, ikiwamo kumsema vibaya.
“Niwashukuru wale wote walioniunga mkono licha ya masimango na matusi waliyoelekezewa,” amesema Mwambe.
Amesema uchaguzi usio na ushindani hutoa viongozi ambao mwisho wa siku hudai kwanza sikutaka au nilishurutishwa.
Mbunge huyo amesema alianza kuona haja ya kugombea baada ya kumshuhudia
Mbowe ambaye ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni akitishia
kuachia nafasi hiyo kwa zaidi ya mara tatu.
“Nilianza kuona nina haja ya kugombea baada ya kumshuhudia Mwenyekiti wa
chama chetu Mh Mbowe akituambia kwamba, asingependa aendelee kuwa
Mwenyekiti wetu na kwamba anatamani angeacha nafasi hiyo kwa mtu
mwingine ili aendeleze yale mazuri aliyafanya, nikaona ipo haja ya
kumpokea kijiti hasa baada ya kueleza kwa kina madhira ambayo amepitia
kwa vipindi vilivyotangulia nikaingiwa na huruma” amesema Mwambe.
Uchaguzi ndani ya chama hicho unatarajiwa kufanyika Desemba 18 mwaka huu
ambapo kwa nafasi ya Mwenyekiti, ni Mwambe pekee amiejitokeza kuchuana
na Mbowe ambaye anatetea nafasi hiyo