Magufuli amesema kuwa askari polisi wanaoishi kwenye nyumba za jeshi
nchini kuanzia sasa hawatatozwa tena kodi ya nyumba na hivyo amewataka
kukaa kwa usalama na kwamba serikali italibeba deni hilo akidai
walikosea kusaini mkataba uliowataka askari hao kulipa kodi.
Ametoa
kauli hiyo leo Jumatatu Novemba 25, alipokuwa akizungumza kabla ya
kuweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa Makao makuu ya Jeshi la
Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
“Kwa
mkataba ambao tulisaini sisi wenyewe ni kwamba nyumba za wanajeshi
zikijengwa watakaokuwa wanakaa huko watakatwa lakini ukweli ni kwamba
hauwezi ukawachukua askari wanaokaa kwenye nyumba ambazo ni kama mahanga
halafu uanze kumtoza fedha, ninafahamu deni hilo ni kubwa lakini
ninawahakikishia kuwa katika nyumba zote zilizojengwa nchi nzima ambao
mkataba wake ulisema wanaokaa mule wakatwe hakuna kukatwa askari yeyote
hilo deni litabebwa na serikali.
“Kabla
sijaja hapa nimeshamwelekeza Waziri wa Fedha na Katibu Mkuu na
ninafikiri kesho au keshokutwa wataanza kulilipia hilo deni ambalo
limeiva na wataanza kulipa zaidi ya Dola za Marekani milioni 25 kwani
deni lenyewe ni kubwa zaidi ya Sh trilioni moja lakini siwezi nikawaweka
maaskari wangu kwenye utumwa wa nyumba za kulala.
“Badala
ya kulala ukaota mabomu na namna ya kupiga risasi unaanza kuota jinsi
ya kulipa deni la nyumba kwa wakati wangu hilo hapana, ni kweli mkataba
ulikosewa lakini siwezi nikakubali makosa ya namna hiyo yakaanza
kufanyika katika kipindi changu kwahiyo maaskari mnapoingia kwenye
nyumba zenu kama una mke wako lala salama,” amesema Rais Magufuli.