Dokta mpango aiomba afdb kujenga barabara njia nne morogoro hadi dodoma

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) akimuomba Mkurugenzi Mtendaji wa
Benki ya Maendeleo ya Afrika- AfDB, Bw. Cheptoo Amos Kipronoh (hayupo
pichani) kuweka katika vipaumbele vya Benki hiyo kwa Tanzania kuhusu
ujenzi wa Barabara ya Morogoro Dodoma yenye upana wa njia nne, kulia ni
Kamishna Msaidizi wa Bajeti Bw. Emmanuel Tutuba.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika- AfDB, Bw. Cheptoo Amos Kipronoh, akieleza nia ya
Benki yake ya kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwemo ujenzi wa
Uwanja wa Ndege wa Msalato Jijini Dodoma, wakati wa Mkutano na Waziri wa
Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani),
Jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa
Benki ya Maendeleo ya Afrika- AfDB, Bw. Amos Cheptoo, baada ya mkutano
uliofanyika katika ukumbi wa Wizara hiyo, Jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha
na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa nne kulia), 
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika- AfDB, Bw.  Amos
Cheptoo, (wa nne kushoto)  wakiwa katika picha ya pamoja na  maafisa
waandamizi wa Wizara hiyo na Benki ya AfDB , Jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha
na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) na   Mkurugenzi Mtendaji
wa Benki ya Maendeleo ya Afrika- AfDB, Bw. Amos  Cheptoo, wakiwa katika
Mkutano Jijini Dodoma. 
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Fedha na Mipango)
Na Benny Mwaipaja, Dodoma
WAZIRI wa Fedha
na Mipango Dkt. Philip Mpango ameiomba Benki ya Maendeleo ya Afrika
kuipatia Tanzania mkopo nafuu kwa ajii ya kujenga barabara ya njia Nne
kuanzia Morogoro hadi Dodoma ili kuboresha usafiri na usafirishaji wa
abiria na mizigo
Dkt. Mpango
ametoa ombi hili Jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki hiyo anayewakilisha
nchi nane za ukanda wa Afrika Mashariki Bw. Amos Cheptoo.
“Barabara hii
ilijengwa muda mrefu miaka ya 80, malori mengi yanapita hapa kwenda
Mwanza, Kigoma na nje ya nchi ikiwemo Burundi, Rwanda, na unaona kabisa
imeelemewa na imeanza kuharibika” Alisema Dkt. Mpango
Alisema amemwomba
Mkurugenzi Mtendaji huyo wa AfDB waanze kuliweka jambo hili kwenye
miradi itakayogharimiwa na Benki hiyo baadae ili barabara hiyo itakayo
kuwa na uwezo wa kuelekeza magari mawili kwenda upande mmoja na mengine
mawili kupita upande mwingine iweze kujengwa.
“Baada ya Dodoma
kuwa Makao Makuu ya nchi, tunahitaji usafirishaji kwa njia ya barabara
uwe na tija zaidi, uende haraka zaidi lakini pia kupunguza ajali. Hivi
sasa kuna ajali nyingi sana kwa sababu magari yanayokwenda Dar es Salaam
na yanayokuja Dodoma au kwenda Mwanza yanapishana kwenye haka kanjia
kamoja” alisisitiza Dkt. Mpango
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Maendeleo ya
Afrika Bw. Amos Cheptoo aliyeko nchini kwa ziara ya kikazi ya siku
mbili, alisema Benki yake itahakikisha Tanzania inapata mikopo ya miradi
yake ya kimkakati na ya kipaumbele ukiwemo huo wa barabara ya Morogoro
hadi Dodoma.
Katika hatua
nyingine Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika- AfDB, Bw. Cheptoo Amos Kipronoh, ameitaka Sekta
Binafsi nchini Tanzania kuchangamkia fursa za mikopo nafuu zilizopo
katika Benki hiyo.
Bw. Kipronoh
alisema kuwa Sekta Binafsi nchini Tanzania ina nafasi nzuri ya kupata
mikopo na utaalam utakaoiwezesha kujikwamua kiuchumi kwa lengo la
kutokomeza umasikini katika Bara la Afrika.
“Sekta Binafsi
hapa Tanzania haijatumia vizuri dirisha la mikopo ya Sekta hiyo
ikilinganishwa nan chi nyingine za ukanda huu wa Afrika na ninakuomba
Mhe. Waziri wa Fedha na Mipango uihamasishe Sekta Binafsi ikope fedha
hizo ili kukuza mitaji yao na kuongeza tija” alisema Bw. Cheptoo
Aidha, alisema
kuwa Benki ya AfDB ipo katika hatua za mwisho za kutoa fedha kwa ajili
ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato Dodoma na tayari
benki hiyo imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara za mzunguko
mjini Dodoma pamoja na miradi mipya ya kuzalisha Nishati ya umeme ambayo
iko mbioni kuwasilishwa katika vikao vya Bodi ya Benki hiyo hivi
karibuni.
Mkurugenzi huyo
amempongeza Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kuwa kiongozi mwenye
maono ambaye amesaidia katika mabadiliko makubwa ya  uchumi na kuzitaka
nchi nyingine barani Afrika kujifunza kutoka Tanzania.
“Nilipotua
nimeona jengo la abiria la III katika Uwanja wa Ndege  wa Kimataifa wa
Julius Nyerere, daraja la juu la Mfugale na ujenzi wa Reli ya Kisasa
unaoendelea kwa kasi, miundombinu ambayo miaka miwili iliyopita
sikuikuta nilipotembelea hapa nchini” alisema Bw. Cheptoo.
Aidha,
amempongeza Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango kwa kusimamia
na kuhakikisha uchumi unaendelea kuwa imara ikiwa ni moja ya lengo la
Benki hiyo katika jitihada za kuifanya Afrika kuwa na uchumi imara.
Kwa upande Waziri
wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, amewataka watanzania kujivunia
hatua za maendeleo zinazoonekana kwa kuwa hata wageni wanaona mabadiliko
makubwa ya kiuchumi nchini.
Ameishukuru Benki
ya AfDB kwa kukubali kufadhili miradi ya barabara za mzunguko Jijini
Dodoma na pia miradi mbalimbali ya kilimo ambayo inaajiri watu wengi,
huku akibainisha kuwa kwa kipindi cha miaka minne miradi mbalimbali
imetekelezwa kwa msaada wa AfDB na kuifanya Tanzania kukua kwa kasi
kiuchumi.
Dkt. Mpango
amewataka watendaji wa Wizara yake kuhakikisha wanawakutanisha viongozi
wa Sekta Binafsi na Watendaji hao wa AfDB kabla ya kumaliza ziara yao
nchini, ili kufanya mazungumzo yatakayosaidia kutumia fursa zilizopo
katika Benki hiyo.
Aidha, Dkt.
Mpango amewataka watanzania wenye vigezo kuchangamkia nafasi mbalimbali
za kazi zinazotangazwa katika Benki hiyo ili kuongeza uwakilishi wa
wananchi hasa kutoka Afrika Mashariki, ikizingatiwa nafasi
zinazotangazwa ni za ushindani.
Benki ya
Maendeleo ya Afrika-AfDB imefadhili miradi 23 hapa nchini ikiwemo miradi
21 ya umma na miwili ya Sekta Binafsi, katika Nyanja za Nishati,
miundombinu ya barabara, usafiri, kilimo, maji na usafi wa mazingira,
yote kwa pamoja ikiwa na thamani ya dola za Marekani bilioni 2 nuta 1