Waziri jafo ameagiza kufukuzwa shule kwa mwanafunzi ambaye ataharibu miundombinu shuleni kwa makusudi

WAZIRI
wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Selemani
Jafo ameagiza kufukuzwa shule kwa mwanafunzi yeyote atakayebainika  
kuharibu kwa makusudi miundombinu au samani  katika shule za umma  kwa
lengo la kuhakikisha usalama wa muda wote wa miundombinu hiyo.


Jafo
ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam jana wakati akizungumza na
waandishi wa habari huku akiwataka wakurugenzi wa mamlaka za Serikali za
mitaa kuhakikisha shule zote katika maeneo yao zimeboresha fomu ya
maelezo ya kujiunga na shule (Joining Instructions)

Alisema
sababu ya kuboresha fomu hizo ni hatua inayolenga kuweka adhabu za
kuchukuliwa dhidi ya mwanafunzi au kikundi cha wanafunzi
kitakachobainika kufanya uharibifu huo.

Alisema
hatua hiyo imetokana  na tabia iliyoanza kujitokeza siku za hivi
karibuni  ikiwemo mkoani Mbeya na Morogoro kwa baadhi ya wanafunzi hao
kufanya uharibu wa miundombinu na samani za shule, jambo alisisitiza
kuwa ni kinyume na utaratibu lakini pia zikirudisha nyuma juhudi za
Serikali na wadau wengine wa maendele katika suala la ujenzi wa shule
hizo.

Alisema
Serikali isingependa kuona uharibifu wa miundombinu hiyo ikitokea kama
walivyofanya wanafunzi wa Shule  ya Sekondari ya Mji Mpya ya Manispaa ya
Morogoro na Shule ya Sekondari ya  Kiwanja  ya Halmashauri ya Chunya
ambao wameonyesha nidhamu mbovu ya kuanza kuharibu miundombinu ya shule
huku akiwapongeza viongozi katika mikoa hiyo kwa kuchukua hatua stahiki.

“Wazazi
na walezi watawajibika kutengeneza kifaa au mali hiyo na kuirejesha
katika hali yake ya awali, aidha mzazi au mlezi wa mwanafunzi
atakayekiuka masharti hayo ya shule, mwanaye asimamishwe masomo au
afukuzwe shule kwa maana hatuwezi kuvumilia kuendelea kuwa na wanafunzi
waharibifu na wasio na maadili mema katika shule zetu” aliongeza Jafo.

Aidha
alizitaka bodi za shule zifanye kazi yao ipasavyo ili kuilinda
miundombinu hiyo na samani za shule na kuwaomba wadau mbalimbali wa
maendeleo kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha maendekeo
ya elimu nchini ikiwa ni pamoja na kusimamia nidhamu ya wanafunzi na
watoto ambao ndiyo nguzo na viongozi wa baadae wa Taifa hili.