Watumishi 44,800 wa kada ya afya kuajiriwa nchini kwa mwaka wa fedha 2019/20 ili kuboresha huduma za afya

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary M.
Mwanjelwa (Mb) akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Silafu Jumbe
Maufi  Bungeni leo jijini Dodoma, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
lililohusu  mpango wa Serikali kuajiri watumishi wa kada ya afya ili
kuboresha huduma za afya nchini.


Happiness Shayo-Dodoma
Serikali imepanga kuajiri
Watumishi 44,800 wa Kada ya Afya kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ili
kukabiliana na changamoto ya uhaba wa watumishi wa kada hiyo na
kuboresha huduma za afya nchini.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst)
Mhe. George Mkuchika wakati akijibu swali la Mhe. Silafu Jumbe Maufi
(Viti Maalum) aliyetaka kujua mpango wa Serikali kuajiri watumishi wa
kada ya afya ili kuboresha huduma za afya nchini.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema,
Serikali ya Awamu ya Tano imeweka kipaumbele cha ajira kwa kada ya afya
na imekuwa ikitoa vibali vya ajira kwa kuzingatia ukomo wa bajeti kuu ya
mshahara na vipaumbele vya mwajiri husika.
Aidha, Mhe. Dkt. Mwanjelwa ameweka
bayana kuwa katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali ilitoa vibali vya
ajira 8,000/= kwa kada ya afya, lakini lengo halikufikiwa kwa sababu ya
kuwepo kwa wataalamu wachache wa kada hiyo waliojitokeza kuajiriwa
Serikalini.
Ili kukabiliana na upungufu wa
Watumishi wa kada ya afya, Mhe. Dkt. Mwanjelwa amewahimiza Wabunge wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwahamasisha wananchi katika majimbo
yao kusoma masomo yatakayowawezesha kuajiriwa katika kada ya afya kwa
lengo la kuwahudumia Watanzania.