Waziri mkuu atoa maelekezo kwa wakuu wa mikoa na wilaya ambao maeneo yao yana upungufu wa chakula

Serikali
imewaagiza viongozi wa mikoa na wilaya watoe taarifa kama maeneo yao
yana upungufu wa chakula na ni kiasi gani kinahitajika.


Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa amesema jana bungeni mjini Dodoma kuwa, wizara ya
Kilimo ikipata taarifa hizo itaratibu vizuri na kuona namna ya kufikisha
chakula kwa wananchi kwa kuwauzia ili zipatikane fedha za kununua
chakula kingine kiwekwe kwenye Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA).

Ameyasema
hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Chemba (CCM) Juma Nkamia
aliyetaka kauli ya Serikali kwa kuwa baadhi ya mikoa ukiwemo wa Dodoma,
Manyara na Singida ina tatizo kubwa la chakula na huenda baadhi ya
wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama hawatoi taarifa sahihi kwa
sababu ya woga.

“Upungufu
wa chakula upo kwa baadhi ya wilaya na maeneo mengine na huu ulitokana
na tatizo la hali ya hewa kwamba yapo maeneo msimu uliopita hayakupata
mvua ya kutosha. Jambo hili linapotokea kule kwenye ngazi hiyo tunao
viongozi…”alisema Waziri Mkuu wakati akijibu maswali ya papo hapo kutoka
kwa wabunge wa Bunge la Tanzania.

“Inapotokea
kama hali ya hewa imekuwa mbaya Mkuu wa Wilaya akieleza atakuwa
anaeleweka kwa sababu pia baada ya kutoa taarifa hiyo timu ya Wizara ya
Kilimo itakwenda kuona hali halisi na kuweza kuzungumza na ile mamlaka
kuweza kupelekewa chakula kwa bei nafuu” alisema.

Alisema
jambo hilo limetolewa ufafanuzi mara nyingi na kwamba, Rais John
Magufuli hajazuia kutolewa kwa taarifa za upungufu wa chakula isipokuwa
kwenye maeneo yenye hali nzuri ya hewa na kila mmoja ana nafasi ya
kulima au kufanya kazi lakini yana upungufu wa chakula.

“Viongozi
waliopo kwenye maeneoi hayo wanao wajibu wa kusimamia kila mmoja
anafanya kazi pamoja na kulima mazao ya chakula na biashara ili waweze
kujipatia tija inapofikia kipindi kama hiki kila mmoja anakuwa na akiba
yake” alisema.

Alitoa mwito kwa wafanyabiashara watumie fursa ya tofauti za hali ya hewa kwenye maeneo kuuza chakula sehemu zenye upungufu.

Aliwataka
wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa wakutane na wafanyabiashara
wawashawishi wapeleke chakula kwenye maeneo yenye upungufu ili kuongeza
vipato vyao.