Mikoa ya kigoma, arusha na kilimanjaro yatajwa kuwa kinara wa uingizaji wa dawa bandia

Na Andrew  Chale 
MIKOA ya pembezoni mwa Nchi ikiwemo ya Kanda ya Magharibi, Kanda ya Ziwa
na ile ya Kaskazini imeripotiwa kuwa  kinara wa dawa duni za binadamu
na mifugo, vifaa tiba na vitendanishi ambavyo havikusajiliwa na Mamlaka
ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA).
Akitangaza matokeo ya operesheni maalum  ya dawa, vifaa tiba,
vitendanishi, dawa asili na tiba mbadala, mbele ya waandishi wa habari
mapema leo Jijini Dar e Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Bw. Akida
Khea   alisema katika zoezi hilo Wilaya zaidi ya 33 katika mikoa 20
wameweza kukamata dawa bandia aina saba zenye thamani ya fedha za
kitanzania Tsh. 12,495,500.
Dawa hizo bandia ni pamoja na  Sonaderm Cream toleo namba A1912 na
A1758, Gentrisome cream (namba GNTRO X030), Sulphadoxine Pyrimethamine
(ilikuwa na namba ya kughushi TAN)
Pia dawa zingine ni  ALPRIM (Sulfamethoxazole 400mg + Trimethoprim 80mg
tablets (namba  6L74) ambapo kiwanda cha Elys Pharmaceutical cha nchini
Kenya kinachozalisha dawa yenye jina kama hilo kimethibitisha kuwa dawa
hizo ni bandia.
Bw. Khea alizitaja dawa zingine kuwa ni pamoja na Homidium Chloride, 
Cold cap ambapo dawa halisi yake ilitambuliwa  kama COLDCAP, na dawa
nyingine bandia ni dawa ya mifugo aina ya TEMEVAC NDV strain 1&2 
ambayo ni chanjo ya kuku  kwa ajili ya ugonjwa wa mdondo.
“katika dawa hizo, uchunguzi wetu baada ya kuzibaini tuliweza
kuwasiliana nawamiliki wa dawa husika ambapo waliweza kututhibitishia
kuwa ni bandia na zingine zimegushiwa maandishi” alisema Khea.
 “Tumebaini mikoa  iliyo pembezoni ikiwemo Kigoma kubainika kuwa na dawa
nyingi bandia pamoja na Mwanza. Lakini pia mikoa ya Kaskazini ikiwemo
Arusha na Kilimanjaro nayo imebainika kuwa na wingi wa dawa hizo”
alisema  Kaimu Mkurugenzi huyo wa TMDA, Akida Khea. 
 Katika tukio hilo TMDA waliwashirikisha mamlaka mbalimbali wakiwemo
Jeshi la Polisi, Msajili wa Baraza la dawa asili na tiba mbadala pamoja
na TAMISEMI.
Nae Mrakibu wa jeshi la Polisi kutoka Makao makuu ya upelelezi kitengo
cha Interpool,  Alekunda Urio  amesema jeshi hilo linafuatilia kwa
karibu na wahusika wote ambao wamebainika katika kuingiza ama kusambaza
watachukuliwa hatua.
“Wajibu wa jeshi la Polisi ni kulinda usalama wa raia na mali zao.
Usalama wa raia ni pamoja na afya za wananchi sisi kama jeshi la polisi
kwa pamoja tunahakikisha usalama wa raia unalindwa na wahusika
watafikishwa kwenye vyombo vya sheria uchunguzi ukikamilika” alisema Bi
Alekunda Urio.
Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA), Akida Khea
akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) mapema wakati wa
kutangaza matokeo ya ukaguzi maalum wa dawa vifaa tiba, vitendanishi,
dawa asili na tiba mbadala, tukio lililofanyika makao makuu ya TMDA,
Mabibo Jijini Dar e Salaam.