Waziri lukuvi aagiza mashamba 24 kilosa kupelekewa ilani ya kufutwa

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi William Lukuvi akizungumza na uongozi wa wilaya ya Kilosa pamoja
na Watendaji wa sekta ya ardhi katika wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro
wakati wa muendelezo wa ziara yake ya kutatua migogoro ya ardhi mkoani
Morogoro.
Baadhi ya watendaji wa sekta ya ardhi
mkoani Morogoro wakimsikiliza Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi William Lukuvi (hayupo pichani) alipokwenda wilayani Kilosa
wakati wa muendelezo wa ziara yake kutatua migogoro ya ardhi mkoani
Morogoro.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi William Lukuvi akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale wakati wa muendelezo wa ziara yake
mkoani humo kutatua migogoro ya ardhi. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya
Kilosa Adam Mgoyi.
Baadhi ya watendaji wa sekta ya ardhi
mkoani Morogoro wakimsikiliza Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi William Lukuvi (hayupo pichani) alipokwenda wilayani Kilosa
wakati wa muendelezo wa ziara yake kutatua migogoro ya ardhi  mkoani
Morogoro.(PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

 

 

Na Munir Shemweta, WANMM KILOSA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi William Lukuvi ameagiza mashamba 24 yaliyopo katika wilaya ya
Kilosa mkoani Morogoro kupelekewa ilani ya kufutwa kutokana na
kutoendelezwa na hivyo kukosa sifa ya kumilikiwa na wamiliki wake.
Lukuvi alitoa agizo hilo leo tarehe 8
Novemba 2019 wilayani Kilosa mkoa wa Morogoro alipozungumza na uongozi
wa wilaya ya Kilosa na watendaji wa sekta ya ardhi katika wilaya hiyo
akiwa katika muendelezo wa ziara ya kutatua migogoro ya ardhi katika
mkoa wa Morogoro.
Alisema, wilaya ya Kilosa haina
kumbukumbu za mashamba jambo lilosababisha wizara yake kuamua kufanya
upekeuzi maalum wa mashamba yote katika wilaya hiyo na kubaini mashamba
24 yasiyoendelezwa tofauti na mashamba 48 yaliyopendekezwa kufutwa
awali.
Kufuatia agizo hilo la Lukuvi, sasa
wilaya ya Kilosa itakuwa na mashamba 72 yanayotakiwa kufutwa baada ya
mashamba 48 ya awali kupendekezwa kufutwa kutokana na kutoendelezwa.
‘’Maafisa Ardhi  wa Wilaya ya Kilosa
mfanye upekuzi wa mashama yote yasiyoendelezwa bila upendeleo wala
kumuangalia mtu usoni na wala msitishwe na mtu yoyote kwa cheo chake au
utajiri wakati wa kufanya kazi hiyo’’ alisema Lukuvi.
Waziri Lukuvi alisema, lengo la
serikali kufuta mashamba yasiyoendelezwa ni kuwafikiria wananchi
wanyonge wasiokuwa na ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo na
kubainisha kuwa mashamba yatakatayofutwa yatagawiwa kwa wananchi na
mengine yatatumika kama ardhi ya akiba itakayotumika kwa shughuli za
uwekezaji.
Aidha, Lukuvi amekemea tabia ya baadhi
ya wananchi wa wilaya ya Kilosa kuuza ama kukodisha mashamba
wanayopatiwa na serikali na kusisitiza kuwa katika kukomesha tabia hiyo
Wizara yake inaangalia namna ya kugawa mashamba yaliyofutwa  kwa vikundi
na kwa wale watakaopatiwa hawataruhusiwa kuuza na kuwataka Maafisa
Ardhi kutofanya uhamisho wa shamba kwa yule aliyepatiwa .
‘’ Mkuu wa Wilaya komesha tabia ya
udalali wa mashamba unaofanywa na baadhi ya wananchi wa Kilosa na yale
mashamba yanayogawiwa kwa wananchi yatumike kwa shughuli
zilizokusudiwa’’ alisema Lukuvi.
Vile vile, Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi ameagiza wafugaji wote wanaomiliki maeneo yenye hati
kuweka uzio katika maeneo yao ili kuepuka mifugo yao kwenda maeneo ya
wakulima na kusisitiza kufanyika ufugaji wa kisasa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya
Kilosa Adam Mgoyi ameomba kufanyika ukaguzi wa ardhi za vijiji kwa kuwa
baadhi yake watu wamejimilikisha, wameuza na mengine kufanyika mgawanyo
usio sahihi. Kwa mujibu wa Mgoyi halmashauri ya wilaya ya kilosa
imeshindwa kufanya uhakiki kutokana na kutokuwa na fedha jambo
alilolieleza kuwa limechangia migogoro ya ardhi katika wilaya hiyo na
kusisitiza kuwa tegemeo la wilaya yake kwa sasa ni mashamba yaliyofutwa
pekee.
Katika hatua nyingine Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amesema vijijji viwili
vilivyosajiliwa katika maeneo ya hifadhi wilayani Kilosa mkoa wa
Morogoro vitaendelea kubaki katika maeneo hayo kufuatia Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kuridhia vijiji 920 vilivyokuwa katika maeneo ya
hifadhi kuendelea kubaki maeneo hayo.
Lukuvi amevitaja vijiji vya Mjambaa
kilichoko katika shamba la Mbugani Estates lenye ukubwa wa ekari 1600 na
kile cha Mambegwa kuwa vitaendelea kutambuliwa na kuagiza  halmashauri
ya wilaya ya Kilosa kwenda kuvipima na kuanisha shughuli za kilimo na
makazi katika vijiji hivyo