John Kaoneka akiendesha darasa, mbele ni wanahabari wakimsikiliza kwa makini
Na Mwandishi Wetu, Arusha
CHAMA cha waandishi wa habari Mkoa wa Arusha (APC), kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Conterpart International lenye makao yake makuu nchini Marekani wameendesha mafunzo kuhusu usalama mtandaoni (Digital Security) kwa waandishi wa habari wanachama wa APC.
Katika mafunzo hayo ya siku tatu yanayoendeshwa na wawezeshaji John Kaoneka na Elie Chansa, kupitia mradi wa Information Safely and Capacity (ISC), waandishi wa habari wametakiwa kuzingatia mafunzo hayo kutokana na umuhimu wake katika utendaji wao wa kazi wa kila siku.
Mratibu wa Chama cha waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha, Seif Mangwangi amewaeleza washiriki wa mafunzo hayo kuwa mafunzo hayo yanafanyika ikiwa ni mwendelezo wa mafunzo ya kwanza ambayo yalifanyika jijini humo kwa baadhi ya waandishi wa habari.
Amesema mafunzo hayo yanayofanyika ni ya awali na kwamba yatafanyika kwa mara nyingine tena kwa lengo la kuwawezesha wanahabari hao kujihami na uvamizi unaoendelea kwenye mitandao na kuweza kufanya kazi zao kwa makini pasipo kuwa na hofu ya kudukuliwa.
Amesema APC imelazimika kuomba mafunzo hayo baada ya kugundua kuwa wanachama wake wamekuwa wakikabiliwa na tatizo kubwa la udukuliwaji wa taarifa zao kupitia mtandao na hivyo kuweka maisha yao katika hali ya hatari.
“Waandishi wa habari wamekuwa katika hali ya hatari sana ya taarifa wanazoandika kudukuliwa na watu wasiokuwa na nia njema, na hivyo kuhatarisha maisha ya wanahabari, baada ya kugundua hili, APC iliamua kuandika andiko kwa wafadhili, Counterpart International na sasa haya ndio matunda yake ambayo mnayapata,”amesema.
Amesema uongozi wa APC utaendelea kutayarisha maandiko mbalimbali kwa wafadhili na kuendesha mafunzo tofauti tofauti kulingana na uhitaji wa waandishi wa habari ili kuwawezesha kufanya kazi ya uandishi wa habari katika hali ya usalama.
Mwezeshaji John Kaoneka amewaeleza waandishi wahabari kuwa uhalifu katika mtandao umekuwa ukikua kwa kiwango kikubwa kila kukicha jambo ambalo kila mtumiaji wa mtandao anapaswa kujihami kwa kujua mbinu za kupambana na wahalifu hao.
|