Waziri lugola aagiza polisi kuwakamata wabadhirifu wa vyama vya ushirika

Na Felix Mwagara, MOHA, Bunda.

WAZIRI
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ameliagiza Jeshi la Polisi
nchini kuwakamata viongozi wa vyama vya ushirika nchini ambao wamekuwa
wakihujumu fedha za wakulima.


Waziri Lugola ametoa kauli hiyo, katika Mkutano wa Viongozi wa Wilaya ya
Bunda, Mkoani Mara, jana, kufuatia Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia
Bupilipili kuwakamata viongozi wa vyama vya ushirika walioshindwa
kurejesha fedha za Serikali zaidi ya bilioni moja na milioni mia nne
atua ambayo imemfanya.
“Nawaagiza Polisi kuendesha operesheni ya kuwakamata wabadhirifu wa
fedha na mali mbalimbali za umma, na agizo hili si la hapa Bunda tu,
bali nchi nzima, makamanda wawasake na kuwatia mbaroni ili iwe fundisho
kwa watu wenye tabia hizo,” alisema Lugola.
Pia Waziri Lugola, alitoa onyo kali kwa viongozi wa vyama vya ushirika
kote nchini kuwa Serikali ya awamu ya tano kupitia Wizara yake
haitamuacha mtu salama atakayechezea fedha za Serikali.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili alisema
wamewakamata viongozi wa vyama vya ushirika walioshindwa kurejesha fedha
za Serikali na watawafikisha mahakamani.
“Fedha za vyama vya ushirika zimeliwa, tukaamua kuwakamata watuhumiwa
wote na tayari tumefanya hizo, na tutawafungulia mashataka ili iwe
fundisho kwa wananchi ambao wanatabia ya kuchukua fedha za umma,”
alisema Lydia.
Waziri Lugola yupo Wilayani Bunda kwa ajili ya ziara ya kikazi,
kuzungumza na wananchi, na pia kutatua kero mbalimbali zinazohusu Wizara
yake Wilayani humo.