Mtatiro atatua mgogoro uliodumu miaka minne


Mkuu
wa Wilaya ya Tunduru , Julius Mtatiro ametatua mgogoro wa muda mrefu
kati ya Wananchi wa kijiji cha Chemchem katika kata ya Tuwemacho dhidi
ya Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ambao ulianza mwaka 2014.



Mgogoro
huo unahusisha madai ya kijiji cha Tuwemacho katika ujenzi wa Barabara
Kuu ya Tunduru Songea na Tunduru Masasi miaka 5 iliyopita ambapo kokoto
zilizokidhi vigezo na viwango zilichimbwa kwenye mgodi wa mawe wa kijiji
hicho kwa ahadi kuwa halmashauri ingelilipa asilimia 20 ya mapato ya
ushuru wa kokoto hizo kwa kijiji husika ambazo ni sawa na shs milioni 48
ambazo kama wangelizipata wangelianza ujenzi wa zahanati kijijini hapo.



Mtatiro
amemwelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Tunduru kuanza mara
moja ujenzi wa zahanati ya kisasa ya shilingi milioni 84 katika kijiji
cha Chemchem kama ishara ya kuwalipa wananchi fedha zao ambazo wamezidai
bila mafanikio, na kwamba fedha hizo zina riba ambayo ni haki ya
wananchi hao.



Pamoja
na hatua hizo, Mtatiro ameelekeza Ofisi ya Mkurugenzi na Ofisa Tawala
wa Wilaya ya Tunduru, waendelee kufanya mawasiliano na TANROAD ili fedha
hizo zipatikane na ameelekeza zitakapotolewa zipelekwe katika kijiji
husika moja kwa moja.



Aidha,
Mtatiro kwa kushirikiana na mbunge wa jimbo la Tunduru Kusini, Mhe.
Mpakate, wameamua kuanzisha ujenzi wa Ofisi ya kisasa ya kijiji ambapo
Mtatiro atatoa mifuko 25 ya Simenti, Mbunge atatoa bati 60 na mifuko 25
ya Simenti na wananchi watachangia nguvu zao.



Katika
mkutano huo, Mtatiro amesisitiza umuhimu wa kuwatendea haki wananchi na
kupambana na shida na kero zao kama anavyofanya Rais Dkt John Pombe
Magufuli.