Yanga yafanyiwa kitu mbaya zambia, yaadhibiwa 2-1 na zesco utd


Mshambuliaji Mnamibia, Sadney Urikhob ameifutia aibu Yanga leo  kwa kuifungua goli moja huku ikishuhudia ikichapwa 2-1 na Zesco mjini Ndola.

BAO la kujifunga la kiungo Mzanzibari,
Abdulaziz Makame dakika za mwishoni limeiondoa Yanga SC kwenye michuano
ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufungwa 2-1 na wenyeji, Zesco
United jioni ya leo Uwanja wa Levy Mwanawasa mjini Ndola, Zambia.

Kwa matokeo hayo, Yanga inatolewa kwa
jumla ya mabao 3-2, kufuatia sare ya 1-1 baina ya timu hizo kwenye
mchezo wa kwanza Septemba 14 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.

Zesco United inayofundishwa na kocha wa
zamani wa Yanga, Mzambia George Lwandamina inaingia hatua ya makundi
inayoshirikisha timu 16, wakati timu ya Tanzania itamenyana na moja ya
timu zilizovuka Raundi ya Pili ya Kombe la Shirikisho kuwania kucheza
hatua ya makundi ya michuano hiyo mingine ya CAF. 

Makame, mchezaji aliyeibukia kikosi cha
vijana cha mahasimu, Simba B kabla ya kwenda kujiendeleza zaidi kisoka
kwao, Zanzibar alijifunga dakika ya 79 alipojaribu kuokoa krosi ya
Kalengo kutoka upande wa kushoto.

Zesco waliuanza vizuri mchezo huo na
kupata bao la kuongoza kupitia kwa mshambuliaji wao Mkenya, Jesse
Jackson Were aliyefunga kwa kichwa dakika ya 25 akimalizia pasi ya
kichwa pia ya Winston Kalengo baada ya mpira wa kurusha wa Simon
Silwimba kutoka upande wa kulia.

Yanga SC wakasawazisha dakika ya 31
kupitia kwa mshambuliaji wake mpya kutoka Namibia, Sadney Khoetage
Urikhob kwa shuti la mguu wa kushoto akimalizia mpira uliopanguliwa na
kipa Jacob Banda, baada ya shuti la Abdulaziz Makame aliyeunga pasi ya
Mghana Lamine Moro kufuatia kona ya Mnyarwanda, Patrick Sibomana kutoka
kushoto.

Baada ya Zesco kupata bao la pili, kocha
wa Yanga, Mkongo Mwinyi Zahera aliingiza washambuliaji Mzambia Maybin
Kalengo, Juma Balinya na Mrisho Ngassa akiwatoa beki Ali Ahmad Ali na
viungo Feisal Salum na Sibomana.

Mabadiliko hayo yaliongeza kasi ya
mashambulizi ya Yanga langoni mwa Zesco United, lakini jioni ya leo
bahati ilikuwa kwa vijana wa George ‘Chicken ’Lwandamina waliofanikiwa
kusonga mbele.

Na pia kutolewa kwa kadi nyekundu kwa
beki Mghana, Lamine Moro aliyeonyeshwa kadi ya pili ya njano dakika ya
90 kulishusha presha ya mashambulizi ya Yanga katika dakika nne za fidia
ya muda uliopotea.

Kikosi cha Zesco United kilikuwa; Jacob
Banda, Mwila Phiri, Clement Mwape, Simon Silwimba, Marcel Kalonda,
Anthony Akumu, Thabani Kamusoko, John Chingandu/Kondwani Mtonga dk63,
Quadri Kola, Winston Kalengo na Jesse Were/Kasumba Umaru dk81.

Yanga SC; Metacha Mnata, Ali Ahmed
Ali/Maybin Kalengo dk84, Ally Mtoni ‘Sonso’, Lamine Moro, Kelvin Yondan,
Abdulaziz Makame, Deus Kaseke, Feisal Salum/Juma Balinya dk82, Sadney
Urikhob, Papy Kabamba Tshishimbi na Patrick Sibomana/Mrisho Ngassa dk87.
Chanzo – Binzubeiry blog