Wahujumu uchumi waanza kuachiwa na kufuatiwa mashtaka tanzania



Hatimae Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imeanza
kutimiza ombi la Rais Magufuli kwa kuwaachia na kuwafutia mashtaka
wafungwa waliokuwa wakikabiliwa na makosa ya uhujumu uchumi.


Leo Septemba 23, Mahakama hiyo imewaachia huru washtakiwa watano
waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwa makosa ya
kujiunganishia bomba la mafuta ambalo ni mali ya Mamlaka ya Bandari
nchini (TPA) kinyume cha taratibu.

Uamuzi huo umefikiwa mara baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini
Tanzania (DPP) kuieleza Mahakama kuwa hana nia ya kuendelea na kesi
hizo.

Walioachiwa huru na mahakama hiyo ni Audai Ismail (43) mkazi wa Kibaha,
Chibony Emmanuel, Roman Abdon, Amina Shaban na Zubery Ally.

Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama hiyo
Januari 16, 2019, kujibu mashtaka matatu likiweno la kujiunganishia
isivyo halali bomba la mafuta mali ya TPA, ambapo kwa pamoja wanadaiwa
kati ya mwaka 2015 hadi Januari 2018 katika eneo la Tungi Muungano
Wilayani Kigamboni, wanadaiwa kujiunganishia bomba la mafuta ya Dizeli

lenye upana wa inchi moja kutoka katika bomba lenye upana wa inchi 24 bila kibali.

Shtaka la pili lilikuwa ni la kuharibu miundombinu kwa madai ya kuwa
walitoboa bomba hilo ambalo lilikuwa likitumika kusafirisha mafuta,
pamoja na kudaiwa kuharibu bomba la mafuta mazito lenye upana wa inchi
28 la kusafirishia mafuta ghafi.