Dpp atoa muongozo kuhusu wahujumu uchumi wanaotaka kusamehewa


Mkurugenzi
wa Mashtaka Nchini (DPP), Biswalo Mganga amesema ofisi yake ipo tayari
kutekeleza ushauri wa Rais  Magufuli aliyetaka kusikilizwa kwa mahabusu
wanaokabiliwa na makosa ya uhujumu uchumi iwapo watakuwa tayari kukiri
na kurejesha fedha za serikali wasamehewe.

Mganga
amesema jambo hilo linawezekana endapo mshtakiwa mwenyewe ataiandikia
ofisi yake barua kupitia kwa Mkuu wa Gereza na kusisitiza kuwa barua
hiyo inapaswa kuandikwa na mtuhumiwa mwenyewe aliye gerezani na siyo
wakili. .

“Utaratibu
ni kwamba, mtuhumiwa mwenyewe aliyeko mahabusu anatakiwa aniandikie
barua kupitia kwa mkuu wa gereza akikiri kosa na kuomba kutubu haraka
iwezekanavyo na sisi tutachukua hatua.
 “Ni
mtuhumiwa mwenyewe ndiye anatakiwa kuandika barua, siyo wakili. Unajua
wakili anaweza kubadilika na hata mtuhumiwa kumkana kuwa sijamtuma
afanye alichofanya kwa niaba yangu, ndiyo maana mara zote watuhumiwa
wanaoomba msamaha na kukiri huandika barua wenyewe kwa mkono wao kupitia
kwa mkuu wa gereza” Amesema DPP Mganga.

Akizungumza
jana wakati wa kuwaapisha baadhi ya viongozi aliowateua, Rais Magufuli
alimuomba DDP ndani ya siku saba kuangalia uwezekano wa kusamehewa
baadhi ya watuhumiwa waliokaa muda mrefu mahabusu kwa makosa ya uhujumu
uchumi endapo watatubu, akisema anatamani kuona Watanzania wote wanaishi
huru ili kushiriki ujenzi wa taifa.