Tatizo la barabara ifakara mlimba kuwa historia

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiongea na wananchi wa Mbingu, Kata ya Igima, wilayani Kilombero, mkoani Morogoro Septemba 15.2019
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,
akiwasalimia  wananchi wa Kata ya Mchombe, wilayani Kilombero, kwenye
mkutano wa hadhara, Septemba 15.2019.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,
akiwahutubia wananchi wa Kata ya Mrimba, wilayani Kilombero, kwenye
mkutano wa hadhara, Septemba 15.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema changamoto ya barabara ya kutoka Ifakara hadi Mlimba iliyokuwa
inawakabili wananchi wa maeneo hayo kwa muda mrefu imepatiwa ufumbuzi
baada ya Serikali kupanga kuijenga kwa kiwango cha lami.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imedhamiria kuboresha
miundombinu ya barabara nchini ikiwemo barabara ya kutoka Ifakara hadi
Mlimba yenye urefu wa km. 126.5.

Waziri Mkuu aliyasema hayo jana
jioni (Jumapili, Septemba 15, 2019) wakati akizungumza na wananchi
katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Matangini, Mlimba
wilayani Kilombero.

“Serikali imedhamiria kuimarisha
barabara katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na ujenzi wa
barabara ya Ifakara-Mlimba kwa kiwango cha lami lengo likiwa ni
kurahisisha usafiri pamoja na kukuza uchumi wa wananchi na Taifa kwa
ujumla.”

Alisema Serikali inatambua umuhimu
wa barabara hiyo kwa ajili ya kuboresha maendeleo ya wananchi na kwamba
itajengwa kwa kiwango cha lami, hivyo aliwataka wananchi hao waendelee
kuiamini Serikali yao.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
alimuagiza Kaimu Ofisa Elimu Mkoa wa Morogoro, Jackson Mpankuli
ahakikishe amepeleka walimu katika shule ya msingi  Matangini na
Mwangazaambazo zinakabiliwa na upungufu wa walimu.

Waziri Mkuu alisema hadi Sepetemba
30 mwaka huu kiongozi huyo awe ameshawahashimia walimu katika shule
husika. Waziri Mkuu alitoa agizo hilo baada ya Mbunge wa Jimbo la
Mlimba, Suzan Kiwanga kulalamikia upungufu wa walimu hao.

Mbunge huyo alisema katika jimbo
kuna tatizo kubwa la upungufu wa walimu hali inayosababisha baadhi ya
wazazi kukodi walimu kwa ajili ya kuwafundisha watoto wao, hivyo Waziri
Mkuu aliagiza walimu wahamishiwe katika shule ndani ya wiki mbili.

Akizungumza na wananchi katika
eneo la Mchombe alipokuwa njiani kuelekea Mlimba, Waziri Mkuu aliwataka
wazazi, walezi na viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero mkoani
Morogoro kuhakikisha wanadhibiti ongezeko la mimba kwa watoto wa shule.

“Lazima kuwalinda watoto wa kike
ili wasipate mimba kwani watashindwa kuendelee na masomo, hivyo
watashindwa kutimiza ndoto zao. Viongozi simamieni utekelezaji wa sheria
kwa kuwachukulia hatua wote waliowapa mimba wanafunzi.”

Wakizungumza kwa nyakati tofauti,
Mbunge wa jimbo la Kilombero, Lijualikali na Mbunge wa Mlimba, Suzan
Kiwanga waliiomba Serikali iwasaidie ujenzi wa barabara za kutoka
Ifakara hadi Mlimba na barabara ya Ifakara hadi Kidatu ambayo ujenzi
wake unasuasua.

Pia Suzan alitumia fursa hiyo
kuishukuru Serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu kwa
barabara ya Ifakara-Mlimba na baadae kuwekwa lami kwa awamu na kusema
kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ikiahidi kitu inatekeleza

Waziri Mkuu anaendelea na ziara
yake ya kikazi mkoani Morogoro ambapo anatarajiwa kutembelea Halmashauri
za wilaya ya Ulanga na Malinyi kukagua miradi ya maendeleo ukiwemo
mradi wa ujenzi wa hospitali ya wilaya na kuzungumza na wananchi pamoja
na watumishi.