Serikali yasikiliza kilio cha wananchi juu ya huduma ya maji njombe

Joctan Agostino, Njombe 

Halmashauri ya mji wa Njombe ipo
mbioni kumaliza changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji bomba, baada ya
serikali kukamilisha usanifu wa ujenzi wa mradi mkubwa wa maji katika mto
hagafilo wenye uwezo wa kuzalisha zaidi ya lita mil 17 kwa siku.

Kwasasa mamlaka ya maji safi na
usafi wa mazingira mjini Njombe NJUWASA imekiri kuwa na uwezo mdogo ambapo
inatajwa kuzalisha lita mil 3 pekee kwa siku, wakati mahitaji ya mji yakiwa ni
lita mil 12 jambo ambalo limeilazimu mamlaka hiyo kufanya mgao wa huduma hiyo
ili kila mtaa uweze kuipata keki ya taifa.

Akizungumzia jitihada zinachukuliwa
na serikali ili kumaliza changamoto hiyo mkurugenzi wa NJUWASA mhandisi John
Mtyauli amesema kipindi kifupi kijacho wakazi wa mji wa Njombe watasahau adha
ya mgao wa huduma hiyo kwani  tayari
serikali kupitia wizara ya maji imeshakamilisha usanifu katika mto Hagafilo
ambao utakuwa na uwezo wa kuzalisha lita mil 17 kwa siku na kumaliza changamoto
ya mgao.

Kuhusu suala la kuongezwa kwa tozo
za maji Mhandisi Mtyauli amesema mamlaka zimelazimika kuongeza kiwango cha tozo
kwa watumia maji ili kuisaidia mamlaka kupata fedha ili kuisaidia mamlaka hiyo
kupata fedha kwa ajili ya kulipa mishahara watumishi wa umma, kuboresha
miundombinu ya mifumo ya maji pamoja na mahitaji mengine ya mamlaka .

Amesema wizara iliyokuwa na dhamana
ya kugharamia mambo yote muhimu katika mamlaka za maji kote chini imejitoa
kwenye jukumu hilo hatua ambayo imezifanya mamlaka kuja na bei mpya ambazo
kiini chake ni mapendekezo ya wananchi kwa lengo la kuzijengea uwezo wa
kujiendesha.

Katika hatua nyingine Wakati
serikali ikifanya jitihada hizo za kuboresha huduma ya maji katika wa Njombe
ambao unatajwa kukua kwa kasi zaidi kiidadi ya watu na kibiashara lakini wakazi
wa mji huo wanasema wameziona jitihada hizo lakini bado kuna dosari katika
utoaji wa huduma ya maji kwakuwa licha ya maji kutoka siku tatu au nne pekee
katika wiki lakini bado tozo zake zimeonekana kuwa juu .

Kufuatia tozo hizo wanaiomba
serikali kupunguza kidogo bei mpya zilizotangazwa ili kuwafanya wananchi kuwa
na uwezo wa kulipa na kuendelea kufurahia huduma ya maji .

Awali tozo za maji ilikuwa ni
shilingi 900 kiwango cha chini huku cha juu kikiwa ni 1100 , wakati bei mpya
kiwango cha chini kikiwa shiling elfu 1449 huku cha juu kikiwa 1632.