Auwsa yapewa siku7 kumrejeshea mteja maji

*NI BAADA YA KUMBAMBIKIZIA ANKARA YA LAKI2 

*MTEJA ASHUKURU, LICHA YA KUTOPEWA FIDIA

Sehemu ya tuzo iliyotolewa

 Na Mwandishi Wetu

Arusha

MAMLAKA ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha (AUWSA), imeamriwa kumrejeshea huduma ya maji mteja wake Erica Charles baada ya kumbambizia bili ya maji ya zaidi ya Shilingi laki2 kwa mwezi mmoja tofauti na matumizi yake ya kawaida.

Katika hukumu iliyotolewa na  bodi ya Mamlaka ya udhibiti wa huduma za Nishati na Maji (EWURA), Februari 29, 2024 na kusomwa Aprili5, 2024 hapa Jijini Arusha na Afisa huduma kwa wateja Kanda ya Kaskazini , Christina Martin,  AUWSA imepewa siku 7 kutekeleza hukumu hiyo na kama Kuna upande ambao haujaridhishwa na hukumu hiyo unaweza kukata rufaa katika tume ya  Taifa ya ushindani.

Kwa mujibu wa uamuzi huo wenye kurasa12, Julai 19, 2023 Erica Silas Charles Mkazi wa Olasiti Jijini Arusha,  alifikisha malalamiko yake kwenye Mamlaka ya udhibiti EWURA dhidi ya AUWSA, akipinga Ankara ya maji ya TZS 253,570.60 sawa na Mita za ujazo 140 ambayo aliipokea mwezi Aprili 2023 kiasi ambacho anadai hakina uhalisia na hakilingani na matumizi ya nyuma ambayo amekuwa akitumia.

Hata hivyo kwa mujibu wa tuzo hiyo iliyosainiwa na Katibu wa bodi ya EWURA Germana Qorro,  juhudi za kutafuta Suluhu ya mgogoro huo ziligonga mwamba baada ya vikao vya tarehe 23 na 29 Agosti 2023 vilivyofanyika katika ofisi za EWURA Kanda ya Kaskazini Jijini Arusha kushindwa ndipo malalamiko hayo yakafikishwa katika ngazi ya usikilizaji.

Katika usikilizaji wa shauri hili Mamlaka ya udhibiti EWURA iliweza kubaini kuwa mtoa huduma Auwsa alitoa dira ya mteja wake Erica Charles kinyume Cha Sheria na kwamba hata pale ambapo mteja alipowasilisha malalamiko yake kuhusu ankara yake kuwa kubwa tofauti na matumizi yake bado watendaji wa Auwsa wakiongozwa na Mhandisi Michael Semba pamoja na Msaidizi wake Bw. Amani walishindwa kumsaidia mteja huyo.

“Inasikitisha kuona kuwa shahidi huyu(Semba), ndiye aliyepokea malalamiko haya lakini ndiye  huyo huyo aliyeelekeza mlalamikaji asitishiwe huduma na kuondolewa dira yake pasipo kushughulikia malalamiko yake, hii ni ama kukosa uwajibikaji au kutumia vibaya Mamlaka dhidi ya mteja,” ilisema sehemu ya tuzo huyo.

Aidha bodi ya EWURA imedai kuwa kwa mujibu wa kanuni ya 47 ya Tangazo la Serikali 849 la 2020, mtoa huduma haruhusiwi kuondoa dira ya mteja kwa kuwa ameshindwa kulipa Ankara . ” Mazingira pekee ambayo mlalamikiwa anaweza kuondosha dira ya Mteja ni pale ambapo usahihi wa vipimo vya dira hiyo unalalamikiwa na hivyo inalazimu dira hiyo kwenda kufanyiwa vipimo maabara kujua kama usomaji wake ni sahihi,”. ilisema tuzo hiyo na kuongeza:

” Hivyo kanuni iliyotajwa hapo juu kamwe isitumike kuondoa dira ya mteja ambaye haijalalamikiwa hata kama masharti ya uondoshaji wa dira hiyo kama yalivyo katika kanuni hiyo yamezingatiwa,”.

Tuzo imeendelea kusema kuwa mlalamikiwa  kupitia mashahidi wake amekiri kuwa aliondoa dira ya mteja kwa taarifa ya kupitia njia ya Simu siku anaondoa dira hiyo na amekiri kuwa dira hiyo  haikufanyiwa vipimo baada ya kuondolewa kwa mteja badala yake ilihifadhiwa ofisini kwa mlalamikiwa.

“Kwa kuzingatia masharti ya kanuni ya 47 na 57, kwa kuzingatia ushahidi usiopingika kuwa dira ya mlalamikaji iliondolewa na huduma kusitishwa bila notisi ya maandishi, pasipo mlalamikaji Wala shahidi wake kuwepo,na pasipo kuwasilisha dira hiyo kwa wakala wa vipimo ili iweze kuhakikiwa  usahihi wake, tunahitimisha hoja hii kuwa zoezi zima halikuzingatia utaratibu wa Sheria na hivyo halikuwa halali,” ilisema tuzo hiyo.

Aidha ikihitimisha hukumu hiyo, bodi ya udhibiti ya EWURA ilimtaka mlalamikiwa AUWSA, kumrejeshea mteja wake Erica Charles  huduma ya maji na kumfungia dira mpya ndani ya siku Saba(7), kuanzia tarehe ya usomwaji wa tuzo hiyo Aprili5,2024, na kwamba mlalamikaji anapaswa kulipa Ankara ya TZS 5346.60 pekee ikiwa ni Ankara ya mwezi Machi ( TZS 2686.60) na Februari 2023 (TZS2686.60) na kila upande uliagizwa kubeba gharama zake.

Akizungumzia hukumu hiyo, Mlalamikaji Erica Charles aliishukuru bodi ya udhibiti ya EWURA kwa kazi nzuri ambayo imeifanya kwa kutoa haki ya kile ambacho alikilalamikia na kusema ijapokuwa bodi hiyo imeshindwa kuitaka AUWSA kumlipa fidia kwa kumsitishia huduma ya maji kwa mwaka mmoja kinyume Cha Sheria  lakini bado haki imetendeka.

“Tuzo imetoka lakini kwa upendeleo kidogo,  Sheria inamtaka AUWSA anilipe fidia licha ya kunirejeshea huduma ya maji, lakini bodi yenyewe haijaona hilo imeamua kunajisi Sheria kwa hapa, nawaomba tu wakati mwingine wasimamie Sheria zote, hii itasaida hizi Mamlaka za maji ziweze kuwajibika ipasavyo,”amesema.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa AUWSA, Meneja uhusiano wa AUWSA, Masoud  Katiba amesema hukumu hiyo ni maelekezo ya chombo kinachoisimamia AUWSA kuweza kutoa huduma bora kwa wateja wake, hivyo wameipokea tuzo hiyo na maamuzi zaidi kuhusu utekelezaji wake yatatolewa baada ya bodi kukaa.